Chongolo: Pimeni maeneo ya kutolea huduma na kuyapa hatimiliki
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Daniel Chongolo ameziagiza Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Ardhi kuweka kipaumbele cha kupima maeneo ya huduma nchi nzima na kutoa hati miliki.
Chongolo ametoa kauli hiyo jana alipotembelea ujenzi wa shule ya Sekondari katika kata ya Mamsera wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro ambapo alisema kuwa, haiwezekani Serikali inashusha fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo alafu tunakaa nazo kienyeji na kuacha kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
Alisema kuwa, kupatikana kwa hati ya maeneo hayo itasaidia yasiingiliwe na kuondoa migogoro isiyo ya lazima hivyo ni lazima kuwekwe programu ya kuhakikisha maeneo yote ya huduma kama shule, Afya ofisi za Serikali na maeneo mengine ya michezo yanapimwa na kuhifadhiwa.
"Hapa mmesema mmechukua eneo kidogo la shule ya msingi na jingine mmenunua kutoka kwa wananchi bila ya kuyapima na kuyaweka kwenye hati ya shule na Halmashauri wakaihifadhi hiyo hati itatokea siku moja kuwa na watoto watakaokuja kusema kiamba chetu kinafika mpaka hapa na kwa sababu hela alichukua baba na hayupo wajukuu wataanzisha mgogoro utakaosumbua watu watakaokuwepo" alisema Katibu Mkuu Chongolo.
Alisema kuwa, endapo hatua hizo hazitachukuliwa itafika wakati kutakosekana maeneo ya kufanyia shughuli za wananchi zitakuja fedha lakini hakuna maeneo na kufanyia miradi hiyo na kupelekea wananchi kukosa fursa.
Katibu Mkuu huyo alisema kuwa, ni lazima tuwe na uchungu na Ardhi iliyoifadhiwa kwa ajili ya maendeleo ya watu wote hivyo tuilinde kama mboni ya jicho ili badae iwasaidie kuleta matokeo kwenye yale matumizi yatakayokuwa yamepangwa katika maeneo hayo na hiyo ndio kazi ya watumishi na watendaji wa Serikali lazima waweke alama kwa kufanya jambo la tofauti.
"Hatuwezi leo eneo kama hili linamiundombinu mizuri na eneo la kisasa lakini tukiulizwa nani anamiliki eneo hili tunaanza kunyoosha kidole halmashauri lakini hati huna akitokea mjanja hapa akapima kwa siri akachukua hati kesho hatuondo... akituondoa haya madarasa na miundombinu hii hatupati hasara kwa uzembe wetu wa kutopima maeneo na kuyaweka kisheria" alisema Chongolo.
Ameitaka Wizara ya Tamisemi kuweka malengo kwa kila Mkurugenzi, Makatibu Tawala mikoa kuhakikisha kwa kipindi fulani kwanza wayatambue maeneo yote na kuyawekea programu ya kila mwaka maeneo kadhaa yapimwe baada ya miaka mitatu maeneo yote yatakuwa yamepimwa na kupatiwa hati.
Alisema kuwa, hawawezi kufanya mambo kwa utamaduni wa zamani sasa hivi wajanja ni wengi tutakuja kujikuta shule za Serikali zinamilikiwa kwenye Ardhi za watu binafsi na halitakuwa sawa kwani kama shule ni ya Serikali ni lazima imilikiwe kwenye Ardhi ya Serikali.
"Nimeona majengo bora na yenye kiwango katika shule hii ya Sekondari lakini kunachangamoto ya eneo la uwanja wa michezo ni lazima mtafute eneo ambalo mtajenga uwanja wa michezo ili vijana na wanafunzi washiriki kikamilifu katika michezo hilo nalo ni somo" alisema Chongolo.
Chongolo alisema kuwa, Serikali inawajibu wa kuwahudumia wananchi na kazi ya ccm ni kufwatilia jinsi huduma zinavyowafikia wananchi hivyo wanataka miundombinu bora itakayowarahisishia wananchi kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Kwa upande wake, Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa CCM, Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga alisema kuwa, hali ya chakula kwa sasa Duniani sio nzuri na Tanzania pia kutokana na sababu ya uchache wa mvua na kuwataka wananchi kutumia vizuri ikiwamo kuhifadhi chakula kidogo walichopata.
"Amani tuliyonayo ni kwa sababu tunashiba kwa sasa hali ya chakula sio nzuri duniani kote na hii ni kutokana na wananchi kuvuna mavuno machache na hili linasababishwa na uchache wa mvua hivyo niwaombe wananchi kile kidogo mlichofuna tukilinde na kuwa makini nacho" alisema Kanali Mstaafu Lubinga.
Naye Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu alisema kuwa, haiwezekani Rais Samia Suluhu Hasani akaleta fedha za kuwaletea wananchi maendeleo alafu atokee mtu na kuharibu fedha hizo hatakuwa tayari katika mkoa huo.
"Nimshukuru Rais Samia Suluhu Hasani kwa imani yake kubwa aliyonionyesha kwake ya kuniteuwa kuwa Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro nimekuja kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya ccm na Serikali ya mama Samia inawapenda watu wote wawe ni ccm au laa na ndio maana imekuwa ikileta fedha mbalimbali za maendeleo na mm nitahakikisha nasimamia fedha hizo bila kumuonea mtu haya" alisema Babu.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa shule hiyo ya Sekondari, Afisa elimu Sekondari wilaya ya Rombo, Petronilla Wakulila alisema kuwa, Serikali ilitoa milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo ya Sekondari ya kata.
Petronilla alisema kuwa, mradi huo ukikamilika utawahudumia wanafunzi 320 wanazotoka katika kata hiyo na pembezoni huku akitoa ombi kwa Katibu Mkuu Chongolo kuongezewa bajeti ya fedha za ujenzi kiasi cha milioni 150 ili kukamilisha miundombinu yote inayohitajika katika maelekezo ya ujenzi.
"Changamoto tuliyokutana nayo katika ujenzi huu ni bei ya vifaa vya ujenzi kuwa juu na hivyo kupelekea gharama ya mradi kuwa kubwa kuliko ilivyotarajiwa na upatikanaji wa eneo la wazi linalotosheleza mahitaji ya ujenzi wa miundombinu yote ya shule" alisema Petronilla.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni