"Misamiati ya Kiswahili imeingizwa kwenye kamusi ya Oxford" Katibu Mtendaji wa BAKITA
Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA,) Bi. Consolata Mushi. |
Na Mussa Augustine.
LUGHA ya Kiswahili imeendelea kutandawaa ulimwenguni kote baada ya toleo jipya la kamusi ya lugha ya kiingereza ya Oxford limeingiza maneno ya Kiswahili takribani mia mbili tofauti na mwaka juzi ambapo kamusi hiyo iliingizwa maneno ya Kiswahili matano pekee.
Hayo yameelezwa leo na Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA,) Bi. Consolata Mushi wakati akitoa mkakati wa utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzanaia Dkt. Philip Mpango katika siku ya maadhimisho ya siku ya Kiswahili ulimwenguni iliyofanyika Julai saba mwaka huu na kuelekeza kuanza rasmi kwa utekelezaji wa matumizi ya lugha ya Kiswahili ili kuendana na maendeleo yake ya kasi ulimwenguni.
''Tunafahamu kamusi ya Oxford inatumika sana duniani, ni kamusi ya kiingereza ila katika toleo hili imehusisha maneno ya Kiswahili mengi zaidi, hii ni tabia ya lugha ya kuchota maneno katika lugha nyingine, na inatupa fahari kubwa na inadhihirisha kuwa Kiswahili kimefika mbali.'' Amesema.
Amesema baadhi ya maneno yaliyoingizwa katika kamusi hiyo ni pamoja na neno 'daladala' likimaanisha magari yanayotumika kusafirisha abiria na 'jembe' kifaa kinachotumika kulimia.
''Maneno yaliyoingizwa katika kamusi hii na kuwa rasmi ni maneno yaliyozoeleka kimatumizi, neno 'chapo' likimaanisha chapati linalotumika sana nchini Kenya limeingizwa katika kamusi hiyo, pia neno 'Mama Ntilie ' limeingizwa katika kamusi ya Oxford kwa maana ya Mama anayepika chakula na kuwauzia watu kwa gharama nafuu ili kila mtu aweze kumudu na kupata chakula, aidha neno 'Singeli' limechukuliwa kama muziki ambao asili yake ni Tanzania, neno 'Kolabo' na 'sambaza' pia yameingizwa katika Oxford...Hii ni dhahiri kuwa Kiswahili kwa sasa kinaenda kwa kasi kubwa.'' Amesema.
Aidha amesema kuwa, Kiswahili kinazungumzwa na watu wapatao milioni 500 duniani msamiati wake unakua na kukuza lugha nyingine na kuingizwa kwa maneno hayo katika kamusi ya Oxford kutasaidia katika kusambaza msamiati wa Kiswahili pamoja na utamaduni wa Mswahili.
''Neno jingine lililoingizwa katika kamusi ya Oxford ni 'chips yai', wengi watataka kufahamu chakula hiki cha chips yai kipoje na kinatengenezwaje tayari tumepeleka utamaduni wa vyakula katika lugha ya kiingereza..Hii ni tija kubwa na fahari kubwa mabaraza yapo kwa ajili ya kutengeneza msamiati ili kusonga mbele zaidi.'' Ameeleza.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni