Rais Samia awapongeza Wakuu wa Shule zinazomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi wa CCM
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewapongeza Wakuu wa Shule zinazomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi wa CCM Tanzania, kwa matokeo mazuri ya mitihani ya kidato cha sita kwa kuondoa alama sifuri.
Hayo yalibainishwa jana jijini hapa na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo wakati akifungua kikao cha wakuu wa shule za sekondari zinazomilikiwa na jumuiya hiyo chenye lengo la kujadili mwenendo wa shule za Chama na namna ya kuboresha taaluma ambapo alitumia nafasi hiyo kutoa salamu za Mwenyekiti wa Chama.
Chongolo alisema Rais Samia alipoelezwa kuhusu yeye (Chongolo) kwenda kwenye warsha hiyo ya walimu wakuu wa shule za jumuiya alihoji maendeleo yake.
“Samia nilipomueleza kuhusu matokeo ya mitihani ya kidato cha sita akaniuliza shule za jumuiya zinaendeleaje, nikamwambia mambo ni mazuri, hazina alama za mwisho.
Nikamwambia asilimia 80 hadi 90 ya wanafunzi waliofanya mtihani wamepata alama za daraja la kwanza, pili na wachache la tatu, akasema angekuja Dodoma kuwapongeza kama angekuwepo,”alisema.
Chongolo aliongeza:”Amenituma kuwaambia kuwa anawapongeza kwa kazi nzuri na kubwa mliyofanya ya kufanikisha matokeo haya,”.
Akitoa hotuba yake, Chongolo aliwapongeza walimu hao kwa kazi nzuri waliyofanya ya kuondoa alama sifuri huku akieleza kama walimu hao wangekuwa sekta ya afya wangekuwa madaktari bingwa.
Alisisitiza kuwa shule hizo zilianzishwa kwa lengo la kuongeza wigo wa utoaji elimu kwa wanaokosa fursa kwenye machaguo ya shule za sekondari, wanaotamani kuendelea lakini hawakufanya vizuri.
Alisema mpaka sasa kazi haijaisha lakini ipo nyingine ya ziada kwakuwa bado lengo la shule kuwezesha vijana kupata fursa ya elimu bora ili kuendeleza ndoto ya kuendelea na masomo upo palepale.
“Fanyeni shule ziingie kwenye ubora wa ushindani sawa na shule nyingine ili wanafunzi wawe na machaguo kwenye shule zetu na ziwe na vigezo vya kupokea wanafunzi,”alisema.
Alisema kwa kiwango hicho kutakuwa na shule za mabingwa zenye kuwaandaa watu ambao hawakuandaliwa vizuri huko chini ili wawe wasomi wazuri.
Alibainisha kwakuwa mitihani ya majaribio iliyotungwa kabla ya wataifa ilikuwa migumu lakini wanafunzi hao walivuna rekodi ya kufanya vizuri ambapo 148 walipata daraja la kwanza lakini ya serikali walipata 423 ipo haja kwa walimu hao kuwaazima kwenye utungaji mitihani.
Aliwataka walimu hao wasihangaishwe na majina ya shule na badala yake waweke heshima zaidi huku akitaka walimu hao kujengewa uwezo zaidi ili wawe na motisha na ari ya kufanya kazi.
“Tusiwachanganye walimu wetu kwa kuwabadilishia vituo vya kazi hivyo maana kuna mabingwa wa kuomba kuhamishwa baada ya kuboronga kwenye eneo lake hivyo tuwalinde,”alisisitiza.
Aidha, Chongolo aliwataka walimu hao kujenga nidhamu ili wasigeuze maeneo ya kazi kuwa ya migogoro na badala yake wakaze buti ili kasi hii iliyopo mwaka mmoja ujao kuwepo wanafunzi wengi hadi kukosa nafasi kwenye shule hizo.
“Heshima ya mwalimu ni matokeo na ukitaka kuheshimiwa tengeneza matokeo mazuri endelea kufanya hivyo na awamu ijayo tutatoa zawadi kwa kiwango cha ushindi uliofanikisha ili ushindani uwe wa kweli,na wenye tija”alisema.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Dk.Edmund Mndolwa alisema jumuiya ya wazazi ilikuwa ni msumari wa moto na unalazimishwa kukaa lakini kutokana na uogozi uliopo sasa jumuiya inaenda vizuri.
Alisema mafanikio yanayoonekana sasa ndani ya jumuiya yanatokana na uongozi mzuri uliopo ambao unahakikisha mambo yote yanayopangwa yanatekelezwa kwa wakati
Alimuomba katibu Mkuu awasaidie kuharakisha muongozo wa kuongoza shule za jumuiya za wazazi upitishwe haraka kwasababu umesheheni mambo mazuri .
“Namshukuru katibu mkuu wa jumuiya ya wazazi kwa kuendelea kupambana na kuhakikisha yale tunayoyapanga yanafanikiwa na ndio maana leo tunajivunia na kufika hapa tulipo, siri kubwa ya matokeo haya yanatokana na utawala bora wa viongozi,”.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni