Wanafunzi waliopata mikopo wa bodi kwa mwaka 2020 hawa hapa, serikali yatumia 464 bilioni kuhudumia mikopo yao
SERIKALI kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)
imetoa orodha ya wanafunzi wa elimu ya juu 47,305 wa mwaka wa kwanza
waliopangiwa mikopo yenye thamani ya bilioni 150.03 kwa mwaka wa masomo
2020/2021 unaotarajiwa kutolewa vyuoni kuanzia wiki ijayo ambapo kati ya
wanafunzi hao wanaume ni 26,964 sawa na asilimia 57.37 na wanawake ni 20,341,
sawa na asilimia 42.63.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi
Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru amesema kuwa Serikali imeongeza bajeti
ya fedha kwa ajili ya wanafunzi watakaonufaika na mkopo ambapo kwa mwaka huu
kiasi kilichotengwa ni shilingi bilioni 464 ambapo ni ongezeko la asilimia 15
ikilinganishwa na mwaka jana.
Badru ameoongeza kuwa HESLB imeshaanza kupeleka fedha za wanafunzi
waliopangiwa mikopo katika vyuo vyao na kuwataka wanafunzi kufuatilia na kupata
taarifa mbalimbali kuhusiana na mikopo yao katika akaunti walizotumia kuomba
mkopo unaojulika kama SIPA (Student’s Individual permanent Account).
“Serikali imeshatupia fedha na tumeanza kuzipeleka vyuoni, lengo letu
ni kuhakikisha wanafunzi wenye sifa wanazikuta fedha vyuoni ambako watajisajili
na kupokea ili watimize ndoto zao.”Amesema Badru
Amebainisha kuwa wanafunzi waliopata mkopo wana sifa zikiwemo kuwa
wahitaji, kuomba kwa usahihi na kuwa na udahili wa chuo kimoja pia orodha ya
awamu ya pili ya wanafunzi waliopangiwa mkopo imepangwa kutolewa siku ya
Jumamosi Novemba 14, 2020 baada ya ya bodi ya mikopo kukamilisha uchambuzi wa
maombi unaoendelea.
Aidha katika mkutano huo Badru amesema kuwa wanafunzi wenye mikopo
wanaoendelea na masomo katika vyuo mbalimbali nchini wapatao 44, 629 wamepangiwa
mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 155.06.
“Wanafunzi hawa 44,629 wamepangiwa mikopo baada ya HESLB kupokea
matokeo ya mitihani yanayothibitisha kuwa wamefaulu kuendelea na masomo katika
mwaka unaoanza , HESLB inaendelea kupokea matokeo ya wanafunzi waliokua na
mikopo mwaka wa masomo uliopita na watapangiwa mikopo.” Amesema Badru
Hata hivyo Badru amewataka waombaji wa mikopo kuwa watulivu wakati wa
upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa kwa awamu inayofuata na amewataka
wanafunzi walionufaika na mkopo wa elimu ya juu kuwa waaminifu na kulipa mikopo
hiyo kwa wakati ili iweze kuwasaidia wanafunzi wengine wenye uhitaji.
“Mnaokopa mnapaswa kurejesha haraka ili pesa hizo ziweze kusaidia na
wadogo zenu na kama mko hapa mchakato wake ni mfupi tu.”Amesema Badru
Hakuna maoni
Chapisha Maoni