Zinazobamba

TUNZENI AMANI-PM






 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na Mufti  na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku (wa pili kushoto) pamoja na  baadhi ya viongozi walioshiriki katika Sherehe za Baraza la Maulid zilizofanyika kwenye  viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam, Oktoba 29, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa rai kwa Watanzania kutunza amani, upendo na umoja miongoni mwao katika kipindi hiki ambacho nchi inaendelea kupokea matokeo ya uchaguzi mkuu wa kutafuta Rais, Wabunge, na Madiwani ambao umemalizika jana.

Waziri Mkuu ametoa wito huo leo (Alhamisi, Oktoba 29, 2020) katika sherehe za Baraza la Maulid, lililofanyika kitaifa Jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Karimjee.

 “Amani ya nchi yetu ni neema kubwa ambayo kila muumini anapaswa kuilinda. Leo hii tumemudu kujumuika pamoja na majirani, ndugu, jamaa na marafiki kufurahia kisomo cha qur’an na kusikiliza nasaha kutoka kwa wanazuoni kuhusu mwenendo sahihi wa Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam kwasababu ya uwepo wa amani”.

Amesema kuwa katika kipindi hiki ni muhimu sana kujiepusha na kauli au vitendo ambavyo vinaweza kupandikiza chuki na uhasama dhidi yetu au waumini wa imani nyingine. “Nitoe rai kwenu viongozi wangu na waumini wenzangu tuendelee kuvumiliana na kustahimiliana hususan pale zinapotokea tofauti miongoni mwetu.”

“Neno amani halitatutoka kamwe, tutaendelea kulitamka neno hili ambalo liliasisiwa na baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na viongozi mbalimbali na Serikali ya Awamu ya Tano tutaendelea kulienzi kwa nguvu zote”.

Vilevile, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kufikisha salamu za pongezi kutoka kwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan za kuwataka waendelee kuliombea Taifa letu sambamba na kusimamia suala la amani, upendo, umoja na mshikamano.

Naye, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir amesema kuwa kwa kipindi kirefu wamekuwa wakisisitiza suala la amani nchini kwani ni kielelezo kikubwa katika kuielezea Tanzania nje ya nchi.

“Amani ya Tanzania ni fahari na ndio nembo kubwa ya Watanzania, tuitunze amani hii na tuwe wakali kukiwa na jambo ambalo linaweza kuhatarisha amani ya nchi yetu”.

Sheikh Mkuu amesema kuwa katika kipindi hiki ambacho tumepita cha uchaguzi Watanzania tunapaswa kukubali matakwa ya Mwenyezi Mungu kwa kuwa yeye ndiye anachagua anachokitaka na anaowataka.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Abubakar Kunenge aliwahakikishia Watanzania kuwa Mkoa wa Dar es Salaam ni salama na ametoa onyo kwa wale wote wenye nia ya kufanya maandamano kinyume na sheria na taratibu za nchi kuacha kufanya hivyo.

 

Hakuna maoni