Viongozi wa dini watoa ya moyoni, waiambia NEC imewatenga
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Rufaa (Mst) Semistocles Kaijage amewaomba viongozi wa dini nchini kuendelea kuhubiri amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Jaji Kaijage ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa Tume na Viongozi wa Dini uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere. Mkutano huo umefanyika ikiwa ni sehemu ya mfululizo wa mikutano ya wadau kuelekea Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika siku ya Jumatano tarehe 28 Oktoba, 2020.
”Nitumie nafasi hii kuwaomba muendelee kuhubiri amani hasa wakati wa kipindi cha kampeni na msichoke kuwasisitiza wagombea, wadau na wananchi kwa ujumla, kuheshimu, kutii na kuzingatia Katiba ya Nchi, Sheria za Uchaguzi, Kanuni na Maelekezo ya Tume.
Tume inatambua kuwa wagombea, wadau na wananchi kwa ujumla ni waamini au waumini wenu, ambao wana wajibu wakuwasikiliza,” amesema Jaji Kaijage.
Aliongeza kwamba Tume inawasihi viongozi wa Dini kuliombea Taifa katika kipindi hiki muhimu, ili utulivu na amani vitawale.
“Tume ina matumaini makubwa ya kufanikisha Uchaguzi huu kwa kutegemea ushiriki wenu katika hatua zote zilizosalia, hadi kufikia siku ya uchaguzi. Imani hii inatokana na ushirikiano mlioonesha hususan wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,” Mwenyekiti wa Tume amewaambia viongozi wa dini.
Jaji Kaijage amewashukuru viongozi wa dini kwa kuwa wepesi wa kuitikia wito, kuwasilisha hoja, kutoa ushauri na kutaka ufafanuzi pale inapohitajika kila wakati Tume inapokutana nao katika vikao mbalimbali.
“Tume itaendelea kuwashirikisha kwa kadri itakavyowezekana. Ahadi ya Tume kwenu ni kwamba itasimamia uchaguzi huu kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni na Taratibu mbalimbali zinazosimamia uendeshaji wa uchaguzi,” Jaji Kaijage amewaambia viongozi wa dini.
Alisisitiza kwamba lengo la Tume ni kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 unakuwa huru, wa uwazi, wa haki na wa kuaminika kwa kuweka mazingira sawa ya ushindani kwa wagombea na vyama vyote vya siasa vitakavyoshiriki.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni