Majaliwa:Serikali inatambua na kuheshimu dini zote nchini na itaendelea kutoa ushirikiano kwa madhehebu yote
By Selemani BETA, Dar es salaam.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa rai kwa viongozi wa dini zote
na jamii kwa ujumla kuendelea kuvumiliana na kustahamiliana hususan pale
zinapotokea tofauti miongoni mwao, lengo likiwa ni kudumisha amani na ulivu
uliopo nchini
Pia Waziri Mkuu, amesema
Serikali inatambua na kuheshimu dini zote nchini na itaendelea kutoa
ushirikiano kwa madhehebu yote katika kutunza na kulinda amani.
Ametoa kauli hizo, Jumapili Februari 16, 2020 kwenye Kumbukumbu
ya Mazazi ya Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam iliyoandaliwa na Nida
Textile Mills (T) Ltd, na kufanyika katika mtaa wa Indira Ghandi jijini
Dar-es-Salaam.
Alisema amani ndiyo msingi wa kila binadamu kufurahia maisha ya
dunia na kufanya ibada zake kulingana na imani yake. “Kwa hiyo,tunapoazimisha
mazazi ya Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam, tuna kila sababu ya
kumuenzi kwa kufuata mafundisho yake.“
Waziri Mkuu amesisitiza kwamba Serikali kwa upande wake
inatambua na itaendelea kuthamini, mchango wa dini, taasisi mbalimbali zisizo
za kiserikali na hata mtu mmoja mmoja katika kutunza na kulinda amani ya nchi
yetu.
“Kuvumiliana na
kustahamiliana ndiko kulikotufanya tuendelee kuwa wamoja na kuitunza neema hii
kubwa ya amani katika nchi yetu. Kila mmoja wetu anapaswa kutambua kuwa anao
mchango mkubwa katika kutunza na kuimarika kwa amani ya nchi yetu.”
Akizungumzia kuhusu maadhimisho hayo ya Mazazi ya Mtume Muhammad
(S. A. W), Waziri Mkuu amesema kwamba hiyo ni fursa muhimu kwa waislamu wote
kuyasoma na kuyatafsiri kwa kivitendo maisha ya Bwana Mtume katika mfumo wao wa
maisha ya kila siku ili kuyafanya maisha yao hapa duniani yawe bora zaidi.
“Tukio hili la leo ambalo nimefahamishwa kuwa linafanyika kwa
mwaka wa 25 sasa, ni kielelezo cha umoja, mapenzi na undugu miongoni mwetu.
Katika Quran Surah ya 49 (Al-Hujurat) ayah ya 10, Mwenyezi Mungu anatufahamisha
kuwa ’hakika waumini ni ndugu.......’ Kwa msingi huo, tukiwa Waislamu suala la
kuimarisha umoja, undugu na ushirikiano katika nyanja zote ni wajibu wa kila
mmoja wetu.“
Kadhalika, Waziri Mkuu ameongeza kuwa Mtume Muhammad (S.A.W)
naye katika kusisitiza suala hilo la umoja, kwenye hotuba yake ya kuaga
alihimiza kuwa mtu yeyote yule hawezi kuwa bora dhidi ya mwingine kwa sababu tu
ya rangi yake au kabila lake lakini kitu pekee kitakachompa yeye daraja hilo la
kuwa bora ni kutenda haki na kumuogopa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Nayei, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakari Bin
Zuberi alisema katika kuadhimisha Mazazi ya Mtume Muhammad (S.A.W)
waislamu nchini wanapaswa waendelee kuwa watulivu na wasikivu wa kila
jambo linalotolewa kwao na viongozi.
Maadhimisho hayo yamehudhuliwa na masheikh na viongozi wa
Serikali kutoka maeneo mbalimbali nchini. Pia yamehudhuriwa na masheikh kutoka
nchi za Paksani, Iraq na Misri ambao kwa ujumla wao wameisifu Serikali ya
Tanzania kwa kudumisha amani, utulivu pamoja na umoja.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni