CCM CHATO YASEMA WAZIRI KALEMANI AMEITENDEA HAKI ILANI
Katibu
wa Siasa na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi, Wilaya ya Chato, Ramadhani
Ndaki, akizungumza wakati wa hafla ya kuwasha umeme katika kijiji cha
Bukamila, Chato. Mgeni Rasmi katika hafla hiyo iliyofanyika Februari 22,
2020 alikuwa ni Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani).
Waziri
wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akifurahia mara baada ya
kuwasha umeme katika kijiji cha Bukamila, wilayani Chato, Februari 22,
2020.
Waziri
wa Nishati Dkt Medard Kalemani akizungumza wakati wa hafla ya kuwasha
umeme katika kijiji cha Bukamila, wilayani Chato, Februari 22, 2020.
Waziri
wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kushoto), akiwatambulisha viongozi
waandamizi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa
Nishati Vijijini (REA), mbele ya wananchi wakati wa hafla ya kuwasha
umeme katika kijiji cha Bukamila, wilayani Chato, Februari 22, 2020.
Kazi
ya kuunganisha umeme katika kijiji cha Bukamila, wilayani Chato
ikiendelea. Taswira hii ilinaswa Februari 22, 2020 wakati Waziri wa
Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), alipokuwa akiwasha rasmi
umeme katika kijiji hicho.
Baadhi
ya viongozi waandamizi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na
Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakimsikiliza Waziri wa Nishati Dkt
Medard Kalemani (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza na wananchi
wakati wa hafla ya kuwasha rasmi umeme katika kijiji cha Bukamila,
wilayani Chato, Februari 22, 2020.
Veronica Simba – Chato
Chama
Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Chato kimekiri kuridhishwa na utendaji kazi
wa Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hilo, Dkt Medard
Kalemani.
Ameyasema
hayo Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM, Wilaya ya Chato, Ramadhani Ndaki
na kuongeza kuwa kwa utendaji kazi wake mahiri, Dkt Kalemani ameitendea
haki Ilani ya Chama hicho ambacho ndicho kinaongoza nchi.
Kiongozi
huyo wa Chama alikuwa akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi
baada ya Waziri Kalemani kuwasha rasmi umeme katika kijiji cha Bukamila,
Kata ya Kigongo, Februari 22, 2020.
“Utendaji
kazi mzuri wa Dkt Kalemani umetupa matumaini sisi viongozi kuwa Ilani
ya Chama inatekelezwa ipasavyo na kwakweli wakati ukifika, tutamtendea
haki,” amesema Ndaki.
Akifafanua
zaidi kuhusu utendaji kazi wa Dkt Kalemani, Ndaki alieleza kuwa, akiwa
ni Waziri mwenye dhamana ya nishati, pamoja na mambo mengine, amefanya
bidii kubwa kuhakikisha wananchi hasa walioko vijijini nchi nzima
wanafikiwa na umeme.
Kwa
upande wa Chato, Ndaki alieleza kuwa Dkt Kalemani amefanya makubwa
katika sekta ya nishati ambapo mpaka sasa Kata zote 23 za Jimbo hilo
zimekwishafikiwa na umeme.
Awali,
akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji hicho cha
Bukamila, Dkt Kalemani alibainisha kuwa hadi sasa jumla ya vijiji
takribani 9,000 vimekwishaunganishiwa umeme nchini kati ya 12,268
vilivyopo, sawa na asilimia 74.
Aliwahakikishia
watanzania kuwa hadi kufikia Oktoba mwaka huu, jumla ya vijiji 10,446
vitakuwa vimeunganishwa na umeme na kwamba ifikapo Juni 2021, vijiji
vyote vya Tanzania Bara vitakuwa vimefikiwa na nishati hiyo.
Alimpongeza
na kumshukuru Rais John Magufuli kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya
kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme nchini na akaahidi kuwa yeye na
viongozi wenzake waandamizi wa Wizara, wataendelea kusimamia vyema
matumizi yake kwa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni