Zinazobamba

TUME YA UCHAGUZI YATANGAZA TAREHE YA UCHAGUZI KWA MADIWANI "WALIONUNULIWA" WA ARUSHA ,SOMA HAPO KUJUA





WAKATI Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema na Mbunge Arumelu Mashariki,Joshua Nassari wakiwa wamewasilisha  ushahidi wa  madiwani waliojizulu huko Arusha kwa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili hatua zichukuliwe kwa madai kuwa madiwani hao wamenunuliwa ili wajuuzulu nafasi zao.
Leo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 43 ikiweni kwenye kata za Madiwani hao,ambapo  uchaguzi utafanyika Novemba 26.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage amesema uchaguzi unafanyika kutokana na sababu kadhaa, ikiwemo madiwani kufariki dunia, kujiuzulu, kutohudhuria vikao na wengine ushindi wao kutenguliwa na Mahakama.

Miongoni mwa kata hizo ni za madiwani waliojiuzulu mkoani Arusha wakieleza ni kutokana na kumuunga mkono Rais John Magufuli.

Jaji Kaijage katika taarifa iliyotolewa leo Jumatano ametangaza uchaguzi huo mdogo baada ya waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kuitaarifu tume uwepo wa nafasi wazi za madiwani katika kata hizo zilizoko katika halmashauri 36 za mikoa 19 ya Tanzania Bara.

Jaji Kaijage amebainisha kifungu cha 13 (1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura ya 292 kinampa mamlaka waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kutoa taarifa kuhusu kuwepo kwa nafasi wazi za diwani au madiwani katika kata husika.

Amesema baada ya kupokea taarifa hiyo na kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 Tume ya Uchaguzi ina wajibu wa kuitisha na kuendesha uchaguzi mdogo katika kata hizo.

"Hivyo, napenda kutumia nafasi hii kutoa taarifa kuwa, tume imepanga kuendesha uchaguzi mdogo katika kata 43 tarehe 26 Novemba, 2017," amesema Jaji Kaijage.

Amesema ratiba ya mchakato wa uchaguzi huo inaanza Oktoba 26 kwa kufanya uteuzi wa wagombea wa udiwani na kampeni zitaanza Oktoba 27 na kumalizika Novemba 25.

Jaji Kaijage amesema vyama vya siasa, wadau wote wa uchaguzi na wananchi wanakaribishwa kwa ajili ya kushiriki kwenye uchaguzi huo.

Ametoa wito kwa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa (madiwani) za mwaka 2015, maadili ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2015 na maelekezo yote yaliyotolewa au yatakayotolewa na tume wakati wote wa uchaguzi mdogo.