TMA YATAKA VYOMBO VYA HABARI KUFUATA WELEDI… YATOA UTABIRI WA NOVEMBA 2017-APRIL 2018
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA) Dk Agnes Kijazi akizungumza katika moja ya mikutano yake (picha ya maktaba) |
NA MAGALI
Vyombo vya habri
vimeshauriwa kufuatilia, kupata na kusambaza taarifa sahihi za mwenendo wa hali
ya hewa ikiwemo tahadhari kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Hayo yamesemwa
na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA) Dk
Agnes Kijazi wakati akizungumza na waandishi habari ofisini kwake kuhusu msimu
wa mvua unaotarajiwa kuanza mwezi Novemba 2017 hadi April 2018.
Dk. Kijazi amesema vyombo vya habari vinapaswa
kushirikiana na wataalamu wa sekta husika katika kuandaa na kusambaza taarifa
za hali ya hewa kwa jamii.
Kwa mara ya kwanza Mamlaka ya hali ya hewa
Tanzania imeweza kutoa utabiri wa mvua za msimu wa mwezi Novemba 2017 hadi
mwezi Aprili 2018 ikiwa ni maeneo mahususi ambayo hupata mvua kwa msimu mmoja
kwa mwaka.
Akitoa utabiri huo kwa waandishi wa habari ,Mkurugenzi
Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi alisema mwelekeo wa mvua za msimu kwa maeneo hayo
unatarajiwa kuwa wa wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya
Dodoma, Singida, Kigoma, Tabora, Rukwa, Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa, Ruvuma,
Lindi na Mtwara pamoja na kusini mwa mkoa wa Morogoro.
Alisema mvua katika maeneo ya mikoa ya Kigoma,
Tabora, Rukwa, Katavi, Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa, Lindi, Mtwara na kusini
mwa mkoa wa Morogoro zinatarajiwa kuanza kunyesha wiki ya kwnza ya mwezi
Novemba 2017 na kusambaa katika mikoa ya Dodoma na Singida ndani ya wiki ya
kwanza ya Desemba 2017.
Dk. Kijazi aliongeza kuwa mtawanyiko hafifu wa
mvua pia unatarajia kujitokeza katika maeneo ya mikoa ya Lindi na Mtwara
kipindi cha Januari hadi Februari, 2018, kipindi ambacho alisisitiza ukanda wa
mvua unatarajiwa kuwa nje ya eneo la kusini mwa Tanzania. “…Mvua zinatarajiwa
kuisha katika wiki ya mwisho ya mwezi Aprili , 2018 katika maeneo mengi
yanayopata msimu mmoja wa mvua. Alisisitiza Dk. Kijazi.
Akizungumzia athari, alisema matukio ya vipindi
vifupi vya mvua kubwa yanatarajia kusababisha mafuriko katika maeneo machache,
na pengine mlipuko wa magonjwa na uhaba wa maji safi na salama hivyo kushauri
mamlaka husika kuchukua tahadhari kukabiliana na hali hiyo.
Pamoja na hayo ameishauri sekta ya afya kuchukua
hatua stahiki kupunguza athari, na kuitaka menejimenti ya maafa na taasisi
okozi kuchukua hatua katika utunzaji wa mazingira, matumizi sahihi ya ardhi na
mipango miji.