Wapinzani kukamatwa Tanzania imekuwa kawaida: Jenerali Ulimwengu
SI ajabu hivi sasa nchini Tanzania kukamatwa viongozi wa upinzani kwa tuhuma za makosa yasiyokuwemo katika vitabu vya sheria na imeanza kuzoeleka kwao kushikiliwa na vyombo vya usalama, anaandika anaandika Mwandishi wetu.
Sasa limekuwa ni jambo la kawaida la kila siku watu kushuhudia kiongozi wa upinzani akikamatwa na polisi kwa tuhuma za makosa yasiyokuwemo katika vitabu vya sheria nchini Tanzania.
Ni jambo ambalo limeanza kuzoeleka kwamba wawakilishi wa wananchi – wabunge au madiwani – wanaweza kushikiliwa na vyombo vya usalama bila kujali kabisa wadhifa wao ndani ya jamii wala usahihi wa tuhuma zinazoelekezwa kwao.
Katika shauri mojawapo, mbunge wa Arusha, Godbless Lema, aliwekwa mahabusu na kushikiliwa kwa muda wa miezi minne bila maelezo yo yote. Hatimaye alipewa dhamana na mahakama ya rufani ambayo iliwakaripia mahakimu wa mahakama za chini pamoja na mawakili wa upande wa mashitaka kwa kile ilichokiita ‘kunajisi sheria’ kwa kuwanyima watuhumiwa dhamana, ambayo ni haki yao ya msingi kabisa.
Ingawaje Lema aliruhusiwa dhamana, amekuwa akilazimika kuhudhuria mahakama mara kwa mara kwa ajili ya kesi zinazomkabili ambazo zinahusu madai ya uchochezi.
Mbunge Ester Bulaya, ameshikiliwa na polisi kwa kushukiwa kutaka kuandaa mkutano wa hadhara nje ya jimbo lake. ‘Kosa’ hili la kushangaza linatokana na amri ya mwaka jana iliyotolewa na Rais John Magufuli kuwazuia wanasiasa kufanya mikutano ya hadhara nje ya majimbo yao ya uchaguzi. Kwamba hakuna sheria inayosema hivyo haionekani kuwasumbua askari-polisi, ambao wanayachukulia matamko ya rais kama sheria ya Bunge.
Tundu Lissu ni mbunge na mwanasheria wa Chadema, chama cha upinzani, na pia ni rais wa Chama Cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS). Hivi sasa amegeuka kuwa mtuhumiwa anayeshikwa mara nyingi zaidi kuliko wengine akituhumiwa kwa mlolongo wa tuhuma, kutoka ‘kumtusi rais’ hadi ‘kutoa matamko ya uchochezi’. Lissu amekuwa akimwita Rais Magufuli ‘dikteta uchwara,’ na hivi karibuni aliingia matatani tena baada ya kujaribu kudhihirisha kwamba Magufuli, alipokuwa waziri wa ujenzi, alichukua maamuzi yaliyosababisha hasara kubwa kwa serikali.
Lissu alichaguliwa kuwa rais wa TLS baada ya Magufuli kueleza kutokupendezwa kwake na chama hicho cha mawakili kuendeshwa na wanasiasa. Tamko la Magufuli lilichochea hamasa kubwa za wanasheria kutoka kila upande wa nchi waliojazana mjini Arusha kumpa Lissu ushindi. Baada ya Lissu kuchaguliwa kwa kishindo, waziri wa serikali alitishia kuifuta TLS, ambacho ni chama cha kitaaluma kilichoanzishwa chini ya sheria za Bunge na chenye uhusiano rasmi wa kikazi na serikali.
Karibu kila siku kuna mwanasiasa wa upinzani anayeamuriwa kupiga ripoti polisi au kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma mbali mbali. Chadema kimedai kwamba tangu Magufuli aingie madarakani zaidi ya viongozi 400 wa Chadema wameshitakiwa kwa tuhuma za kubuni, na mara nyingi wamenyimwa dhamana.
Kwa jinsi ambavyo wanasiasa wa upinzani wanavyobughudhiwa na polisi, na kuitwa mara kwa mara vituoni kutoa maelezo, mtu mmoja ameshauri wapinzani wafungue tawi dogo katika vituo vya polisi ili waweze kuendesha shughuli zao kwa urahisi zaidi.
Chama kingine cha upinzani, Civic United Front (CUF), kimeingia katika mgogoro wa kiuongozi ambao wengi wanaamini unachochewa na serikali. Mgogoro mkubwa ni kati ya Profesa Ibrahim Lipumba, (mwenyekiti aliyejiuzulu kisha akabadili uamuzi wake na kudai kurejea katika nafasi hiyo), na Seif Sharif Hamad, ambaye ni katibu mkuu wa CUF na mpinzani wa siku nyingi mwenye ushawishi mkubwa za kisiasa visiwani Zanzibar
Katika mvutano huo, asasi za kiserikali zinaonekana kumuunga mkono Profesa. Msajili wa vyama vya siasa ameonyesha kubariki kufukuzwa kwa wabunge waliomuunga mkono Hamad na pia ameidhinisha Lipumba apewe fedha za ruzuku ambazo ni halali ya CUF.