TGNP YALIA NA MFUMO KANDAMIZI KWA WANAWAKE NDANI YA VYAMA VYA SIASA,SOMA HAPO KUJUA
MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) umesema mifumo kandamizi iliyopo katika siasa unamnyima mwanamke haki ya uongozi na ushiriki katika shughuli za kidemokrasia.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TGNP, Vicensia Shule (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari leo kuzungumzia Tamasha la Jinsia la mwaka 2017 linalotarajia kuanza rasmi Septemba 5 hadi 8 ya mwaka 2017 katika viwanja vya TGNP Mabibo jijini Dar es Salaam.
Aidha umesema hali hiyo inasababisha uwepo wa idadi ndogo ya wanawake katika nafasi za uongozi na maamuzi kuanzia serikali za mitaa hadi serikali kuu, Bunge, Mahakama na nyadhifa nyingine.
Hayo yameelezwa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Vicensia Shule.
Akizungumza na waandishi wa habari juu ya Tamasha la Jinsia la 14 la Siku Nne, litakalofanyika kuanzia kesho hadi Septemba 8 mwaka huu lenye lengo la kujadili changamoto zinazomkabili mwanamke za kiuchumi, kisiasa na kijamii na jinsi ya kuzitatua.
Amesema kuwa kikwazo hicho kinatokana na vyama kutokuwa na miongozo ya viwango vya uwakilishi kwa jinsia huku akibainisha kuwa mfumo uliopo na kwamba kila chama kina utaratibu wake wa kupendekeza wagombea ambao mara nyingi unakosa uwazi na unagubikwa na rushwa ya ngono.
“Mara nyingi wanawake na wasichana wamekuwa wakibaguliwa kwenye sehemu za afya, elimu, uwakilishi wa kisiasa, soko laajira na kwengineko. Hali hii inakuwa na athari hasi kwa maendeleo ya vipaji vyao na uhuru wao wa kuchagua,” alisema Shule.
Akizungumzia kuhusu tamasha hilo, Shule amesema tamasha la mwaka huu litalenga kujenga mikakati ya muda mrefu ya mageuzi ya mifumo hiyo kandamizi.
Tamasha litakuwa na mada ndogo ndogo tatu ambazo ni uongozi na maendeleo, haki ya kiuchumi kwa mwanamke na wanawake historia yetu.
Ametaja malengo makuu ya tamasha hilo kwa mwaka huu kuwa ni kutafakari na kusherehekea mafanikio, changamoto zilizopo katika kuendeleza usawa wa kijinsia, wakizingatia utekelezaji wa mikataba, maazimio, sera na mikakati mbalimbali ya kimataifa, kikanda na kitaifa.
Mengine ni kutathimini ushiriki wa wanawake katika michakato ya kufanya maamuzi katika uongozi wa kisiasa kwenye serikali za mitaaa. Kufuatilia, kuhifadhi, kutambua na kusherehekea viongozi wanawake wenye michango ya kuigwa juu ya usawa wa kijinsia na uwezo wa wanawake, hususani mapambano dhidi ya mfumo dume na uliberali mamboleo.
Pia imo kuimarisha harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi kupitia ujenzi wa nguvu za pamoja.
Aidha Shule amesema pia wadau watapata kubadilishana uzoefu, kujengeana uwezo, kutafakari na kusherehekea changamoto na mafanikio katika kufikia usawa wa kijinsia.
N