TUNDU LISSU ATIKISA BARA LA AFRIKA ,AWA GUMZO KILA KONA,SOMA HAPO KUJUA
Wakati wenzao wakisema makosa manne ndiyo yanayoweza kumlazimu mtuhumiwa kupimwa mkojo, Jumuiya ya Afrika Mashariki imesema inafuatilia sakata la mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi.
Lissu, ambaye ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alikamatwa Alhamisi akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wakati akisubiri kwenda Kigali, Rwanda kuhudhuria mkutano wa jumuiya hiyo.
Wanasheria wa Lissu wamesema waliambiwa na polisi kuwa amekamatwa kwa tuhuma za uchochezi, lakini alitakiwa kutoa kipimo cha mkojo, jambo ambalo limezua maswali.
“Tutafanya mipango ya kufuatilia kesi ya Wakili Tundu pamoja na mchakato mwingine wowote wa mahakama ambao umeshafikishwa mahakamani au unaweza kufikishwa mahakamani, kwa niaba yake kuthibitisha haki za Mtanzania kama zilivyoelezwa na sheria ya kimataifa,” inasema taarifa ya Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki (EALS) iliyosainiwa na rais wake, Richard Mugisha.
Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa EALS inachukulia kukamatwa kwa Lissu kama ishara nyingine ya kuendelea kuzorota kwa uhusiano baina ya Serikali na TLS, hali iliyoanza wakati wa uchaguzi wa viongozi wa chama hicho.
“Ni kitu kilicho wazi kuwa uhusiano huo umekuwa ukiharibika tangu kipindi cha kuelekea na baada ya matokeo ya Mkutano Mkuu wa mwaka wa TLS ambao Wakili Lissu alichaguliwa na wanasheria wenzake kuongoza TLS kwa mwaka mmoja,” anasema Mugisha.
Wakati EALS ikitoa msimamo huo, wanasheria nchini bado wanahoji sababu za Lissu kuchukuliwa kipimo cha mkojo wakati akituhumiwa kwa makosa ya uchochezi.
Kwa mujibu wa wanasheria hao, makosa yanayoweza kusababisha mtuhumiwa achukuliwe kipimo hicho ni ya usalama barabarani, matumizi ya dawa za kulevya, ubakaji na mashauri ya ndoa na watoto ambayo hulazimu mkemia kupima sampuli hizo.
Lakini Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa alisema uchunguzi wa polisi hauna mipaka na kwamba jeshi hilo halifanyi kazi kwa mihemko ya watu, bali kwa kuzingatia weledi.
Alisema kitendo cha watu kuhoji suala la Lissu kupimwa mkojo ni kuingilia uchunguzi. Alisema uchunguzi ni suala pana, hivyo kuwataka wasubiri mtuhumiwa huyo atakapofikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka yake.
“Kwenye suala la ku-suspect (kutuhumu), polisi anaweza ku-suspect anything (kitu chochote) kutoka kwa mtu yeyote. Siwezi kuelezea mikakati na mbinu za kiuchunguzi, lakini mtambue kwamba uchunguzi is too general (ni mpana), unaweza kuchunguzwa kwa mambo mengi,” alisema Mwakalukwa.
==>Hapo chini kuna tamko la Wanasheria Hao
==>Hapo chini kuna tamko la Wanasheria Hao