Mahakama ya Rufaa yakubali rufaa ya DPP Dhidi ya Masheikh wa Uamsho
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ameshinda rufaa dhidi ya viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), Sheikh Farid Hadi Ahmed na wenzake 21 wanaokabiliwa na mashtaka ya ugaidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
DPP alikata rufaa Mahakama ya Rufaa akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu, kuhusu mamlaka ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kusikiliza na kutoa uamuzi wa hoja walizoziibua washtakiwa kupitia kwa mawakili wanaowatetea, baada ya kusomewa mashtaka yanayowakabili.
Siku waliposomewa mashtaka, washtakiwa kupitia mawakili, Juma Nassoro na Abubakar Salim pamoja na mambo mengine walihoji uhalali wa Mahakama ya Kisutu kusikiliza shauri lao, pia waliiomba mahakama iwafutie mashtaka wakidai kulikuwa na kasoro za kisheria.
Mahakama ya Kisutu katika uamuzi wake ilikataa kusikiliza hoja za washtakiwa hao, ikisema haina uwezo wa kisheria kusikiliza hoja zozote kutoka kwao kwa kuwa mashtaka yanayowakabili yanasikilizwa na Mahakama Kuu tu, hivyo ikawaelekeza kuwasilisha hoja hizo Mahakama Kuu.
Washtakiwa hawakuridhika na uamuzi wa Mahakama ya Kisutu, hivyo walifungua maombi ya mapitio Mahakama Kuu, wakiiomba mahakama iitishe na kuchunguza kumbukumbu za mwenendo wa kesi hiyo ili kujiridhisha na uhalali na usahihi wake.
Walidai Mahakama ya Kisutu ina mamlaka ya kusikiliza na kutoa uamuzi wa hoja walizoziibua baada ya kusomewa mashtaka.
Mahakama Kuu katika uamuzi uliotolewa na Jaji Fauz Twaib ilikubali hoja za mawakili wa washtakiwa kuwa Mahakama ya Kisutu ina uwezo wa kusikiliza na kutoa uamuzi wa hoja zao na alielekeza mahakama hiyo kuendelea na usikilizwaji wa uamuzi wa hoja za washtakiwa hao.
DPP hakuridhika na uamuzi huo hivyo alikata rufaa Mahakama ya Rufaa, akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu.
Mahakama ya Rufaa katika hukumu iliyoandikwa na Jaji Bethuel Mmila kwa niaba ya wenzake, Jaji Kipenka Mussa na Jaji Rehema Mkuye waliounda jopo lililosikiliza rufaa hiyo, imetengua uamuzi wa Mahakama Kuu.
Hukumu hiyo imesomwa leo na Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufaa, Phocus Bampikya ikisema Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina uwezo wa kusikiliza na kuamua hoja zilizoibuliwa na washtakiwa hao kupitia kwa mawakili wao.
Mahakama ya Rufaa imesema hakuna sharti lolote kisheria linaloipa mamlaka mahakama hiyo kusikiliza na kutoa uamuzi wa hoja hizo na kwamba, mahakama hiyo ina uwezo wa kuwezesha mshtakiwa/washtakiwa kusomewa au kuwezesha kusomewa maelezo ya mashahidi tu kabla ya kwenda kusikilizwa na Mahakama Kuu.
Imesema manufaa ya matakwa hayo ya mahakama kuwezesha mshtakiwa kusomewa maelezo ya mashahidi ni kuwafanya kujua mapema aina ya ushahidi utakaotolewa dhidi yake wakati wa usikilizwaji Mahakama Kuu na watakaotoa ushahidi huo ili kupata nafasi nzuri ya kuandaa utetezi wake.
“Ni mtazamo wetu kwamba mambo/hoja zilizoibuliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ni za kisheria ambazo Mahakama ya Hakimu Mkazi haina mamlaka kuyaamua. Masuala hayo yanapaswa kusubiri na kuibuliwa Mahakama Kuu wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo,” inasema hukumu hiyo.
Mahakama hiyo imeelekeza Mahakama ya Kisutu kuendelea na shauri hilo kuanzia pale lilipokuwa limeishia kabla ya kufunguliwa kwa mapitio Mahakama Kuu