Home
/
Unlabelled
/
SAKATA LA UTEKAJI LAJITOKEZA KWENYE MAHUBILI YA VIONGOZI WA DINI KWENYE IBADA ZA BASAKA,SOMA HAPO KUJUA
SAKATA LA UTEKAJI LAJITOKEZA KWENYE MAHUBILI YA VIONGOZI WA DINI KWENYE IBADA ZA BASAKA,SOMA HAPO KUJUA
ASKOFU DK. SHOO
VIONGOZI wa dini wamekemea vitendo viovu vilivyoanza kushamiri katika jamii ya Watanzania vikiwamio utekaji, ubinafsi na tamaa ya kung’ang’ania madaraka.
Akihubiri katika Ibada ya Kitaifa ya Ijumaa Kuu iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Moshi Mjini, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Shoo alisema katika baadhi ya nchi za Afrika, viongozi wamekuwa wagumu kuachia madaraka huku wengine wakilazimisha kuongezewa vipindi vya uongozi.
Dk. Shoo ambaye pia ni Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, alikemea tabia za ubinafsi, ukabila na matumizi mabaya ya madaraka miongoni mwa viongozi wa Afrika na kwamba zinarudisha nyuma maendeleo na kuwanyima haki wananchi.
Alisema mambo hayo yanaweza kusababisha mahangaiko na mifarakano miongoni mwa wananchi wa Afrika na kwamba viongozi wanaoendekeza vitendo hivyo wanapaswa kupata uponyaji na kukubali toba ya kweli.
Alisema hatua hiyo imekuwa ikisababisha umwagaji damu kwa wananchi wasio na hatia na viongozi wanaohusika wamekuwa hawajutii matokeo ya kung’ang’ania kwao madaraka.
“Kuna dhambi za aina tatu au nne hivi. Afrika inatawaliwa na ubinafsi, kukosa uzalendo na watu hawatamani maendeleo. Wako wanaofanya usanii na wanaachia rasilimali za taifa zinaporwa na wanaoitwa wawekezaji,” alisema.
“Kuna baadhi ya nchi kama Burundi na pale (Jamhuri ya Kidemokrasi ya) Congo. Viongozi wamegoma kuondoka madarakani na kutaka kuongezewa muhula. Matokeo yake wananchi wanakufa lakini wanafurahi tu. Huu ni ubinafsi, viongozi wanajijali wao badala ya wananchi waliowachagua kuwaongoza.
Katika mahubiri hayo, alisema mambo yanayoendelea katika la Bara la Afrika hivi sasa hayaakisi yale tunayoyafanya na kibaya zaidi ni matumizi mabaya ya madaraka. Alisema hata maandamano ya raia yanayoendelea nchini Congo kupinga uteuzi wa Waziri Mkuu ni matokeo ya kupuuzwa kwa ushauri wa viongozi wa dini.
“Haiwezekani viongozi wanakaa kwenye madaraka na anajiona yeye ndiye yeye. Mtu anamaliza muda wake hataki kuondoka. Yanayoendelea Kongo na kwingineko ni matokeo ya kupuuza ushauri wa viongozi wa dini,” alisisitiza.
Pia alikemea baadhi ya viongozi wa dini ambao wamekuwa wakitoa mafundisho ya uongo kama vile kutangaza kuwaombea waumini ili wafanikiwe bila kufanya kazi huku msisitizo wao ukiwa kutoa sadaka ya fungu la 10. Alisema huo ni usanii ambao viongozi wenye tabia hiyo wamekuwa wakitumia kama njia ya kujitajirisha.
Alisisitiza kuwa njia pekee ya Watanzania kujikwamua na umaskini na kujiletea maendeleo ni kufanya kazi na wananchi wanapaswa kuachana na ulaghai unaofanywa na baadhi ya viongozi wa dini.
Alisema Rais Dk. John Magufuli anapaswa kupongezwa na yeye binafsi anamsifu na kumuunga mkono kwa juhudi zake za kuhamasisha maendeleo kwa Watanzania, kwa kuwa yatakuja kwa kujituma kufanya kazi kwa bidii.
Kutokana na kauli za Rais magufuli kutaka watu wafanye kazi, alisema Watanzania wanahitaji kutubu ili wabadilike na kuwa na roho ya kujituma na kupenda kufanya kazi.
Alisema maandiko matakatifu yanasema roho ya uvivu ni dhambi ambayo kwa mwanadamu haifai na anahitaji kuondokana nayo pamoja na kuacha njia za mkato za kujipatia fedha, maarufu kama ‘kupiga dili’.
“Neno la Mungu linasema fanyeni kazi, na si kukaa chini, pia si tu ili mradi unatoa fungu la 10, fanyeni kazi ambayo italeta mabadiliko na maendeleo,” alisema.
AKEMEA UTEKAJI
Askofu wa Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT) ya Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Dickson Chilongani, amekemea kushamiri kwa matukio ya uhalifu, yakiwamo ya utekaji na kuwataka Watanzania kumwomba Mungu awaepushe na vitendo hivyo.
Akizungumza katika ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Anglikana mjini Dodoma, alisema vitendo hivyo pamoja na kusababisha hofu, Watanzania wanapaswa kumwomba Mungu ili yasitokee.
Dk. Chilongani aliwataka viongozi wa dini kutotumia muda wao mwingi kwenye masuala ya siasa na kusema jukumu lao ni kuwa karibu na waamini wao ikiwa ni pamoja na kuwatoa hofu na vitisho vilivyotawala.
Alisema jukumu la viongozi wa dini ni pamoja na kuwaonea huruma na kuwaombea watu wanaowaudhi kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kuyatii makusudi ya Yesu kufa msalabani.
MALASUSA ANENA
Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa, aliwataka wananchi kuishi kwa upendo, kusameheana na kuachana na vitendo vya kusalitiana.
“Pilato alishindwa kuchukua hatua na matokeo yake akawa anawafurahisha watu. Kulikuwa na sauti nyingi zikisema asulubiwe Yesu, akaamua kusikiliza sauti hizo si kila sauti za watu wengi ni za Mungu kwa wakati wote… sio mambo yote yanayoamuliwa kwenye kura ni halali,” alisema
Aidha, alisema wakati Yesu anasulubiwa aliwaombea msamaha kutokana na udhaifu wetu.
“Hapa Yesu alitufundisha pendo lake, wanaokufanyia mabaya haijalishi ni kitu gani unatakiwa kuwasamehe hatutakiwi kuwa na chuki kwani kufanya hivyo ni dhambi,” alisema
Malasusa alisema pamoja na Yesu kupigwa aliwaombea msamaha, hivyo mkikubali kusamehana hata kanisa linakuwa katika sehemu ya furaha.
CHENGULA ASISITIZA HAKI
Naye Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo LA Mbeya, Evarist Chengula, akihubiri katika ibada ya Ijumaa Kuu, iliyofanyika katika Parokia ya Mwanjelwa, aliwataka viongozi mbalimbali nchini kutenda haki na kuepuka uonevu.
Alisema viongozi mbalimbali wanatakiwa kutenda haki na kuhukumu kwa haki badala ya kuwaonea wanyonge.
“Wakati tunakumbuka mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye alihukumiwa bila kosa, tujaribu kuwaelekeza wengine ambao wamegubikwa na tabia ya uonevu na dhuluma na kutofuata ukweli, kuepuka matendo hayo ili kuishi katika ukristo,” alisema.
Askofu Chengula alisema kuelekea huruma ya Mungu ni kugeuka na kuacha mambo yanayowakosesha haki wanyonge na viongozi waombeane kutafuta ukweli katika kuhukumu watu.
SAKATA LA UTEKAJI LAJITOKEZA KWENYE MAHUBILI YA VIONGOZI WA DINI KWENYE IBADA ZA BASAKA,SOMA HAPO KUJUA
Reviewed by Unknown
on
15:40:00
Rating: 5