Zinazobamba

MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA AONYWA,KAMATI YA BUNGE YASEMA ANAVUNJA SHERIA KUHUSU MGOGORO WA CUF,SOMA HAPO KUJUA

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, imemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa kuzingatia sheria katika kushughulikia mgogoro wa uongozi ndani ya Chama cha Wananchi (CUF).

Hatua hiyo imekuja wakati viongozi wa CUF wakiwa katika mvutano mkali, huku upande mmoja ukimkataa Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti wa chama hicho wakati Msajili wa Vyama vya Siasa akimtambua kuwa mwenyekiti halali licha ya kujiuzulu nafasi yake wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015.

Jana, Mbunge wa Madaba, Joseph Mhagama (CCM), akisoma taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria juu ya utekelezaji wa bajeti ya ofisi ya waziri mkuu kwa mwaka wa fedha 2016/17 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2017/18, alisema mgogoro huo wa CUF unaweza kusababisha athari za Muungano.

Mhagama aliyekuwa akisoma hotuba hiyo kwa niaba ya Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohamed Mchengerwa, alisema: “Katika mgogoro unaoendelea ndani ya CUF, Kamati inashauri Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuchukua jitihada za kutosha kusuluhisha mgogoro huo ili kuepusha athari kubwa zinazoweza kujitokeza katika Muungano.

 “Kamati inaiagiza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na weledi katika kusimamia na utoaji wa ruzuku kwa vyama vya siasa na kuhakikisha kwamba taratibu hizo zinafuatwa katika utoaji ruzuku kwa vyama vya siasa.”

Wakati akisema hayo, wabunge wa CUF ambao wanamuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, walizungumza na waandishi wa habari na kumtaka Msajili wa Vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi kuacha kuingilia na kuchochea mgogoro ndani ya chama hicho kwani hana mamlaka ya kuwachagulia viongozi.

Akizungumza kwa niaba ya wabunge wengine, Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya chama hicho ambaye pia ni Mbunge wa Tandahimba, Ahamad Katani, alisema CUF inapingana na Jaji Mutungi kuingilia utendaji, uamuzi na shughuli za chama hicho.

“CUF inapita katika mazingira magumu, Msajili anaendelea kutumika vibaya kutugawa wapinzani, tunamwomba asimamie haki,” alisema.

Kuhusu utendaji kazi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kamati hiyo ya Bunge ya Sheria na Katiba, ilishauri tume hiyo kuchukua jitihada za kutosha katika uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura.

“Hatua hizi zijumuishe utoaji wa elimu ya uraia, hususan uandikishaji wa wapigakura kwa vijana wengi zaidi ili waweze kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura au kupigiwa kura,” alisema Mhagama.



HOTUBA YA WAZIRI MKUU

Katika hotuba yake ya bajeti, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema ofisi yake inaomba kuidhinishiwa Sh bilioni 121.65 kwa ajili ya Bunge kati yake Sh bilioni 114.45 zikiwa za matumizi ya kawaida na Sh bilioni 7.2 matumizi ya maendeleo.

Kwa upande wa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake, aliliomba Bunge kuidhinisha Sh bilioni 171.66 kati yake Sh bilioni 74.64 matumizi ya kawaida na Sh bilioni 97.02.

Awali akizungumzia utekelezaji wa bajeti ya ofisi yake kwa mwaka 2016/17 na mipango ya mwaka 2017/18, pamoja na mambo mengine, alisema Serikali itahakikisha watumiaji wa lugha za alama wanapata haki ya kupata habari na vituo vyote vya televisheni vimeelekezwa kutumia wakalimani wa lugha ya alama.

“Napenda kuvikumbusha vituo vyote vya televisheni kuweka wakalimani wa lugha katika vituo vyao. Katika mwaka 2017/18 Serikali itaendelea kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kutoa vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye ulemavu shuleni na vifaa vya kufundishia,” alisema Majaliwa.

Akizungumzia ajira, alisema hadi kufikia Machi mwaka huu, jumla ya ajira 418,501 zimezalishwa nchini.

Kati ya ajira hizo 239,017 sawa na asilimia 57 zimezalishwa katika sekta binafsi wakati ajira 179,484 sawa na asilimia 43 zimezalishwa kutokana na shughuli za sekta ya umma ikiwamo miradi ya maendeleo.