FREEMAN MBOWE AMKABA KOO WAZIRI MKUU BUNGENI,NI KUHUSU VYAMA VYA UPINZANI,SOMA HAPO KUJUA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais,
Dkt. John Magufuli hajawahi kutangaza ama kutoa kauli ya kufutwa kwa vyama vya
siasa nchini.
Ametoa kauli hiyo leo (Februari, 2, 2017) Bungeni
mjini Dodoma wakati akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni,
Mheshimiwa Freeman Mbowe katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu.
Katika swali lake Mheshimiwa Mbowe alisema Rais
Dkt. Magufuli alinukuliwa akisema atahakikisha anafuta vyama vyama vya
upinzani na ifikapo mwaka 2020 hakuna upinzani nchini.
Pia Mheshimiwa Mbowe alitaka kujua nini kauli ya
Serikali kuhusu kunyimwa dhamana kwa Mbunge wa Arusha Mjini, Mheshimiwa
Godbless Lema ambaye anashikiliwa kwa muda miezi mitatu.
Mbali na Mheshimiwa Lema, pia kiongozi huyo alitaka
kujua kuhusiana na kufungwa kwa Mbunge wa Kilombelo, Mheshimiwa Peter
Lijualikali pamoja na madiwani sita wa chama hicho ambao wamefungwa na viongozi
wengine 215 wanakabiliwa na kesi mbalimbali.
“Kwanza nataka nikanushe kwamba Mheshimiwa Rais
hajawahi kutangaza kuvifuta vyama vya upinzani. Pia Watanzania wote wanajua
nchi hii inaongozwa kwa sheria, kanuni na taratibu i,” amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa “tunajua katika kuendesha
nchi tunaendesha kwa mihimili mitatu ipo Serikali, Mahakama na Bunge na hakuna
mhimili unaoweza kuuingilia mhimili mwingine,”.
“Pia Watanzania wote wanajua kwamba jambo lolote
ambalo lipo Mahakamani haliwezi kuzungumzwa mahali pengine popote, hivyo siwezi
kutumia nafasi hii kuzungumzia mambo yote yanayoendelea chini ya sheria na
yaliyo mahakamani,” amesema.
Wakati huo huo; Waziri Mkuu amewahakikishia
Watanzania kwamba suala la upungufu wa sukari halitatokea nchini kwa sababu viwanda
vya ndani vinaendelea kuzalisha na hadi mwishoni mwa Januari vilifikia asilimia
86 ya uzalishaji.
“Hadi kufikia mwishoni mwa msimu wa uzalishaji ambao
ni mwezi Machi, tunaweza kuwa tumefikia malengo na kama itajitokeza upungufu
Serikali itatafuta namna nzuri ya kupata sukari kwa kushirikiana na wenye
viwanda nchini,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali
la Mbunge wa Mvomero, Mheshimiwa Suleiman Sadiq aliyetaka kujua hali ya sukari
ilivyo nchini kwa sasa na hatua gani zinazochukuliwa na Serikali ili kunusuru
hali ya uhaba wa sukari isijitokeze.