Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ataja sababu vyakula kupanda bei sokoni........Asisitiza Tanzania Haijakumbwa na Baa la Njaa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema nchi haijakumbwa
na baa la njaa na amewataka Watanzania kutosikiliza kampeni za upotoshwaji
zinazofanywa na baadhi ya wafanyabiasha kuhusu hali ya chakula kwani si za
kweli bali ni za uzushi zenye lengo la kupandisha bei za vyakula.
Amesema Serikali ndio yenye jukumu la kutoa taarifa
za kuwepo kwa njaa ama kutokuwepo na kwamba taarifa zinazosambazwa za kuwepo
kwa baa la njaa nchini hazina ukweli wowote na Serikali inawahakikishia
wananchi kuwepo kwa usalama wa chakula.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Januari
16, 2017) wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa Dodoma baada ya
kuzindua safari za ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutoka Dar es
Salaam kwenda Dodoma, ambapo amesisitiza kwamba hali ya upatikanaji chakula
nchini ni tofauti na inavyoelezwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo baada ya kutolewa kwa
taarifa katika vyombo mbalimbali vya habari kuhusu kuwepo kwa baa la njaa
nchini jambo ambalo si la kweli. Amewataka wananchi kuwa watulivu na jambo hilo
likitokea Serikali itatoa taarifa.
“Mwaka jana nchi ilikuwa na akiba ya
chakula cha zaidi ya tani milioni tatu hali iliyopelekea baadhi ya Wabunge na
wafanyabiashara kuomba kibali cha kuuza nafaka nje ya nchi, ambapo Serikali
ilitoa kibali hicho baada ya kujiridhisha kuwepo kwa akiba ya kutosha ya
chakula,” amesema.
Amesema baada ya kutolewa kwa kibali hicho tani
milioni 1.5 ziliuzwa nje ya nchi na Kiasi cha tani milioni 1.5 zilizobaki
zilihifadhiwa kama akiba ambapo tayari wameruhusu ziuzwe hapa nchini ili
kupunguza kupanda kwa bei za vyakula nchini.
“Naomba wananchi msiwe na wasiwasi juu
ya hali ya chakula nchini. Msisikilize kelele zinazopigwa na watu mbalimbali
pamoja kwenye baadhi ya vyombo vya habari yakiwemo magazeti kwani taarifa hizo
si za kweli. Chakula kipo cha kutosha licha ya mvua kusuasua katika baadhi ya
maeneo nchini,” amesema.
Hata hivyo Waziri Mkuu amesema kuwa kwa sasa mvua
zimeanza kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo amewaomba wananchi
kuzitumia kwa kulima mazao ya muda mfupi yanayostahimili ukame.
Waziri Mkuu amesema kwamba endapo kutatokea uhaba wa
chakula nchini, Serikali itatoa utaratibu wa namna ya upatikanaji wa chakula
kwa wananchi wake.
Kuhusu kupanda wa bei ya vyakula katika baadhi ya
masoko amesema inatokana na kuwepo kwa uhaba wa chakula katika nchi jirani.
Aidha, Waziri Mkuu amesema kwamba Wizara ya Kilimo,
Mifugo na Uvuvi, itatoa taarifa kuhusiana na hali halisi ya chakula nchini kwa
sasa na pia itatoa taarifa kuhusu hali ya mvua ili Watanzania waweze kupata
ukweli wa hali ilivyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,