WATANZANIA WAKIMBILIA KENYA ,NI BAADA YA BALAA LA NJAA KULIKUMBA TAIFA,SOMA HAPO KUJUA
HALI ya njaa inayoelezwa kuwepo hapa nchini kwa sasa
inadaiwa kusababisha baadhi ya Watanzania kuvuka mpaka na kuingia nchini Kenya
kusaka chakula, anaandika Charles William.
Taarifa
kutoka Wilaya ya Longido mkoani Arusha zinaeleza kuwa, wafugaji katika eneo
hilo kwa sasa wanalazimika kwenda Kenya kutafuta malisho ya mifugo yao huku pia
upatikanaji wa chakula kwa wananchi ikiwa ni shida.
Akizungumza na MwanaHALISI Online kwa njia ya simu,
Lepilall Ole Moloymet, Luteni Mstaafu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), mkazi wa
Longido ambaye pia amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo amedai kuwa hali yao ya
chakula ni mbaya kufuatia njaa iliyosababishwa na ukame.
“Tuna hali mbaya sana huku, Serikali imetutelekeza,
hatuna Mbunge kwasababu aliyekuwepo wamemvua ubunge na matatizo tuliyonayo
hakuna wa kuyasemea. Wananchi tunahangaika, mifugo inakufa hovyo na tumeamua kuihamishia
Kenya,” amesema.
Luteni Ole Moloymet ambaye ni mkazi katika kijiji
cha Isinya wilayani Longido amesema ukame umesababisha mifugo ya wananchi kufa
kwa kukosa malisho na hivyo kulazimika kuvuka mpaka na kuingia nchini Kenya ili
kunusuru mifugo hiyo.
“Hakuna mvua. Wafugaji tunahangaika tumehamisha
mifugo karibu asilimia 80 kwenda nchi jirani ya Kenya, tunaomba serikali
itusaidie kwani hata upatikanaji wa chakula kwa wananchi wa wilaya hii ni mgumu
sana,” amesema.
Hata hivyo, Daniel Chongolo Mkuu wa Wilaya ya
Longido alipotafutwa na mtandao huu kuhusu suala hilo, amesema Serikali
inachukua hatua madhubuti ili kushughulikia tatizo la ukame wilayani Longido.
“Wananchi wa wilaya hii kwenda nchini Kenya mara kwa
mara si ajabu kwani wanaishi eneo linalopakana na nchi hiyo ingawa ni kweli
kumekuwa na ukame. Awamu hii mvua haijanyesha kwa wingi wilayani hapa na hata
maeneo mengine ya nchi tofauti na miaka iliyopita.
Suala lingine ni kuwa, mifugo imekuwa mingi kuliko
ukubwa wa eneo la wilaya hii kwahiyo lazima pawe na uhaba wa malisho. Hata
hivyo, sisi kama serikali tupo katika mpango wa kutafuta mbegu za kuotesha
majani ili tuzimwage katika maeneo mbalimbali kwasababu kwa sasa majani hayaoti
yakatoa mbegu, yakiota tu mifugo inayala yote,” amesema Chongolo.
Kuhusu uhaba wa chakula kwa wananchi, Chongolo
amesema kwamba asilimia 90 ya wananchi wa Longido ni wafugaji na wanategemea
chakula kutoka nje ya wilaya hiyo, hivyo wananchi ni kawaida wananchi hao kuuza
mifugo ili waweze kununua chakula.
“Ni asilimia tano tu ya wananchi wa Longido ndiyo
wakulima. Asilimia 90 ni wafugaji na wanategemea chakula kutoka nje ya wilaya.
Ni sawa na maeneo ya wakulima, kwa mfano Njombe ukitaka kupata nyama lazima
uuze mahindi ukanunue nyama,” amesema.
Chongolo ameeleza kuwa kuna tatizo la wafugaji
kutonunua chakula cha akiba wakati ambao magunia ya mahindi yanakuwa
yanapatikana kwa bei rahisi na hivyo kujikuta katika wakati mgumu wakati ambao
bei ya mahindi inakuwa imepanda.
“Tatizo linakuja pale chakula kinachosafirishwa
kutoka wilaya zingine kuja hapa kinapopanda bei, ndiyo maana tupo kwenye
mchakato wa kutengeneza sheria ndogo (by laws) kupitia Halmashauri ya Longido
itakayolazimisha wananchi wa jamii ya wafugaji kuwa na akiba ya chakula ambacho
watanunua wakati wa mavuno,” amesisitiza.