USHINDI WA CCM UCHAGUZI MDOGO WAMPA JEURI RAIS MAGUFULI,SOMA HAPO KUJUA
Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais John Magufuli
amesema ushindi wa CCM wa ubunge na madiwani katika Uchaguzi Mdogo uliofanyika
juzi nchini ni ishara ya ushindi wa chama chake katika uchaguzi ujao kutokana
na wananchi kuonesha imani kwake na serikali yake.
Rais Magufuli aliyasema hayo kwa waandishi wa habari
muda mfupi kabla ya kumpokea Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan aliyefika
Ikulu, Dar es Salaam jana akiwa kwenye ziara yake ya siku mbili nchini.
Rais Magufuli alisema ushindi huo ni kipimo cha
utendaji wake kwa wananchi na hivyo umemuongezea ari ya kuwatumikia wananchi
kwa moyo wake bila ya kujali changamoto mbalimbali zilizopo.
“CCM Oyee! Mnaonaje ushindi wa CCM? Hii
inadhihirisha ni namna gani wananchi walivyo na imani na mimi na serikali
yangu. Tumeshinda ushindi wa kishindo katika kata na Jimbo, wenyewe mmeshuhudia
namna tulivyowapiga. Au mnasemaje?” Rais Magufuli
aliwaambia waandishi wa habari na kisha akawashukuru na kuelekea eneo lake
maalumu akimsubiria Rais wa Uturuki kwa ajili ya kumpokea.
CCM mbali ya kushinda kiti cha ubunge cha Dimani
visiwani Zanzibar, imeshinda kata 18 kati ya kata 20 zilizofanya Uchaguzi Mdogo
wa Udiwani juzi kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za kufa kwa waliokuwa
wakishikilia nyadhifa hizo na kufutwa kwa matokeo kwa amri ya mahakama.
Kata ambazo CCM imeshinda ni Nyarenanyuki (Arumeru,
Arusha), Isegehe (Kahama, Shinyanga), Nkome (Geita), Kiwanja cha Ndege
(Manispaa Morogoro), Lembeni (Mwanga, Kilimanjaro), Ihumwa (Dodoma), Matevez
(Meru, Arusha), Kimwani (Muleba, Kagera), Igombavanu (Iringa), Kijichi (Mbagala,
Dar es Salaam), Ng’hambi (Dodoma), Kinampundu (Singida), Kasansa (Katavi),
Malya na Kahumulo (Mwanza), Mkoma (Mara), Misugusugu (Kibaha, Pwani).
Aidha, CCM imeshindwa katika Kata ya Duru mkoani
Manyara, ambako mgombea wa Chadema, Ali Shaaban ameibuka mshindi.