BAADA YA KUANGUKA VIBAYA KWENYE UCHAGUZI MDOGO,VYAMA VYA UPINZANI VYAFUNGUKA,SOMA HAPO KUJUA

MWENYEKITI WA CHAMA CHA WANANCHI CUF NAYE AFUNGUKA HAYA
Na. Julius S. Mtatiro
Goodmorning. Katika uchaguzi huu mdogo CUF ilikuwa
inatetea kata 1 ya Kimwani Muleba na CHADEMA ilikuwa inatetea kata 1 ya Duru,
Babati. Kata zingine zote zilikuwa za CCM na zilikuwa zinatetewa na CCM.
Matokeo yanaonesha CCM imetetea viti vyake vyote vya
udiwani (takribani 20), CUF imenyang’anywa kiti chake kimoja (Kimwani) na
CHADEMA imelinda kiti chake kimoja (Duru).
Kwa vyovyote vile vyama mbadala haviwezi kujivunia
matokeo haya kwani havikuweza kuishinda CCM, na CCM haina cha kutambia kwani
imeongeza kata moja tu. Kwa sasa nina mambo kadha ya kuzungumza;
Hali halisi inaonesha kuwa kama vyama mbadala
vingeshirikiana vingelishinda kata si zaidi ya 7 hivi. Bahati mbaya
mashirikiano haya yalikosekana tangu mwanzo baada ya upande wa “CUF ya Msajili
na Bwana Yule” kusisitiza kuwa wataweka wagombea nchi nzima na hakuna UKAWA.
Lakini pia, hata shajihisho la ushirikiano mkubwa
zaidi lililokuja kuzuliwa na kaka yangu Prof. Kitila Mkumbo lilifanywa TOO LATE
kwa lengo la kutafuta sababu ya kujificha baada ya matokeo. Niliwahi kusema, kiuzoefu
vyama haviwezi kuachiana maeneo wiki moja kabla ya siku ya uchaguzi na kushauri
hivyo si kwa nia njema.
Baada ya CUF ya Msajili na Bwana Yule kujipanga
kuvuruga uchaguzi huu na kushusha spirit ya UKAWA, vyama vya NCCR na CHADEMA
pia vilionelea kila kimoja kijipiganie jambo ambalo ni kosa kubwa. Na madhara
ya migawanyiko yote yalijulikana.
Uzoefu unaonesha kuwa, kuishinda CCM kwenye chaguzi
ndogo ni nadra mno. Kuliwahi kuwa na mfululizo wa chaguzi ndogo, Tarime,
Busanda, Tunduru, Mbeya Vijijini n.k. na kote huko CCM ilishinda isipokuwa
Tarime na baadaye Arumeru. Katika chaguzi ndogo CCM hutawanya rasilimali zake
nyingi zikajaa kwenye majimbo au kata hadi POMONI.
Mkakati wa DOLA na CCM kuvitumia baadhi ya vyama au
baadhi ya viongozi kwenye vyama (mamluki) unaelekea kufanikiwa sana. Lakini,
sera za “Self Protectionism” ndani ya vyama mbadala hata kwenye mambo
yanayohitaji ushirikiano wa kitaifa zitaendelea kuvigharimu vyama vyetu.
Good News kwa ACT Wazalendo kwamba huenda ndicho
chama kilichofanikiwa kwenye uchaguzi huu kuliko vyama vyote (CCM inclusive)
kwani pamoja na uchanga wake kimevishinda baadhi ya vyama vikongwe kwenye kata
chache (kwa idadi ya kura na si ushindi wa jumla). Na hiyo ni alert call kwamba
ACT is needed in the UKAWA basket na kwa hiyo ianze ku BEHAVE like a true party
wakati UKAWA pia ikiiandalia mazingira kisaikolojia.
Bado CCM inashinda chaguzi kwa kutumia mifumo ilele;
rushwa, mabavu, hila, wawakilishi wa NEC na NEC yenyewe, uwezo wa uelewa wa
wapiga kura (Mfano. CCM imepeleka uandikishaji wa Bima ya Afya kwa wananchi
kata ya Nkome, wakati wa uchaguzi = Rushwa).
Vyama vya upinzani vinashindwa chaguzi hizi kwa
sababu ya kukosa ushirikiano wa kweli baina ya vyama hivyo, maelezo namba 7
hapo juu na sentensi ya kwanza ya maelezo yaliyo namba 5 hapo juu.
Kwa hakika, matokeo haya hayana athari zozote za
kufaulu kwa Magufuli katika sera zake au kushindwa kwa Magufuli katika sera
zake. Yaani, CCM ya Magufuli haijawa na ushawishi wa ziada kwa wapiga kura ili
kupata ushindi huu kwenye ngome zake. CCM bado inashinda chaguzi kibabe na kwa
mkakati dola zaidi bila kujali nani yuko madarakani.
Sijaona connection yoyote kati ya matokeo haya na
siasa za 2020. Vyama vyote vinayo fursa ya kuendelea kujipanga na kama
tutafanikiwa kuuvunja mfumo dola unaoathiri vyombo vya uchaguzi na uhuru wake,
unaoondoa mazingira sawa kwa vyama kufanya siasa n.k, mabadiliko ya kikatiba
kwenye NEC na sheria za uchaguzi na mengine mengi, siasa za 2020 zitakuwa
mbichi sana.
TUNDU LISSU WA CHADEMA NAYE ASEMA HAYA BAADA YA UCHAGUZI HUO WA MARUDIO,
Na. Tundu Lissu
Waheshimiwa na makamanda poleni kwa mapambano na hongereni kwa kazi kubwa mliyoifanya kwenye chaguzi hizi. Naona kila mmoja wetu anasikitika jinsi matokeo ambavyo yamekuwa tofauti na matarajio yetu na kazi tuliyoifanya.
Waheshimiwa na makamanda poleni kwa mapambano na hongereni kwa kazi kubwa mliyoifanya kwenye chaguzi hizi. Naona kila mmoja wetu anasikitika jinsi matokeo ambavyo yamekuwa tofauti na matarajio yetu na kazi tuliyoifanya.
Ni rahisi, katika mazingira haya ya kushindwa na
kabla vumbi halijaisha, kuanza kulalamika, kunyoosheana vidole na kukatishana
tamaa. Hii haitusaidii sana. Badala yake, tunachohitaji zaidi ni
‘brainstorming’ kuliko ‘blamestorming.’ Naomba nifanye ya kwanza. Chaguzi ndogo
za ubunge au udiwani ni ngumu sana kushinda katika mazingira halisi ya nchi
yetu.
Mifano michache inathibitisha ukweli huu. Katika
election cycle ya ’05-’10, tulishinda Jimbo la Tarime lakini tukapigwa
Biharamulo Magharibi na Busanda. Tarime lilikuwa Jimbo letu tangu Uchaguzi Mkuu
wa ’05, Busanda lilikuwa la maCCM na Biharamulo Magharibi lilikuwa la TLP.
Sikumbuki vizuri kama tulishinda Kata hata moja katika mzunguko wa uchaguzi wa
kipindi hicho.
Katika election cycle ya ’10-’15, tulipigwa Igunga
licha ya kazi kubwa tuliyofanya, lakini tukashinda Arumeru Mashariki iliyokuwa
chini ya maCCM. Vile vile tulishindwa Kalenga, Chalinze na Ulanga Magharibi
yaliyokuwa ya maCCM tangu Uchaguzi Mkuu wa ’10.
Kwenye chaguzi za Kata za ’12 kama mnakumbuka, licha
ya kazi kubwa na rasilimali nyingi, tulipata Kata tatu tu kati ya 26 zilizokuwa
zinagombaniwa. Ukiachia Ifakara Mjini ya Mh. Juakali, Kata nyingine mbili –
Kiboriloni na Iseke – zilikuwa zetu tangu Uchaguzi Mkuu wa ’10.
Kwa mantiki hii, matokeo ya jana sio ya kushangaza
sana. Kata ya Duru ilikuwa ya kwetu na tumeitetea, nyingine zote tulikopigwa zilikuwa
za maCCM. Hatujanyang’anywa iliyokuwa yetu, hatujanyakua zilizokuwa zao. Hata
hivyo, funzo kubwa zaidi la historia ya chaguzi hizi ni hili hapa: licha ya
kupigwa kwenye chaguzi ndogo hizi, tumeendelea kufanya vizuri zaidi katika kila
Uchaguzi Mkuu uliofuatia kipigo cha chaguzi ndogo.
Mwaka ’10 tulifanya vizuri zaidi licha ya kupigwa
Busanda na Biharamulo Magharibi katika mzunguko wa ’05-’10. In fact, tulichukua
Jimbo la Biharamulo Magharibi mwaka huo. Na tulipata Kata nyingi zaidi ’10
kuliko ilivyokuwa ’05. Mwaka ’15 tulipata ushindi mkubwa zaidi katika Kata na
majimbo licha ya kupigwa kwenye chaguzi ndogo za mzunguko wa ’10-’15.
Hoja yangu hapa ni kwamba uchaguzi wa marudio hauna
direct and negative bearing kwenye matokeo yetu ya Uchaguzi Mkuu unaofuatia. On
the contrary, uchaguzi wa marudio unatupa fursa ya kupanda mbegu ambayo,
ikitunzwa vizuri, inakuwa na mazao bora kwenye chaguzi zinazofuatia.
Kwa upande mwingine, chaguzi za marudio – kwa sababu
ya udogo au uchache wa maeneo yanayogombaniwa – yanawapa maCCM fursa ya kutumia
nguvu kubwa za rasilimali na za kidola ukilinganisha na tunazotumia sisi.
Kwenye Uchaguzi Mkuu unaofuatia, nguvu hizo zinasambazwa nchi nzima na kwa hiyo
effectiveness yake inapungua.
Ndio maana tumefanya vizuri zaidi kwenye Uchaguzi
Mkuu kuliko kwenye chaguzi ndogo za marudio. Hili, kwa maoni yangu, ndilo
fundisho kuu la chaguzi hizi za marudio. Hatuna sababu kubwa ya kushangilia
kutokana na matokeo ya jana. Hata hivyo, hatuna sababu yoyote ya kuomboleza
pia. Obviously, maCCM na wapambe wao wataandika ‘wasifu wa marehemu’ wa
CHADEMA/UKAWA na kuutangaza dunia nzima na kwa sauti kubwa. Hilo lisitupofushe
macho yetu, hata kama linakera sana.
Tutathmini kazi tuliyoifanya na matokeo
tuliyoyapata. Tupate mafundisho sahihi ya kazi hiyo na matokeo yake. Tutumie
mafundisho hayo kwa kujipanga vizuri zaidi kwa ajili ya ‘the real prize’: 2020.
ZITTO KABWE NAYE AFUNGUKA NA KUSEMA HAYABAADA YA UCHAGUZI HUO WA MARUDIO,
Nachukua fursa hii kuwapongeza Sana kwa kazi kubwa
mliyoifanya kwenye chaguzi ndogo za udiwani na ubunge zilizomalizika hivi punde
nchi nzima. Ingawa hatukushinda hata kata moja katika kata 20 zilizokuwa
zinashindaniwa, lakini tumefanya vizuri kwenye matokeo.
Chama chetu kilisimamisha wagombea katika Kata 5
kati ya Kata 20 nchi nzima, Isagehe (Kahama), Kijichi (Dar es salaam), Kiwanja
cha Ndege (Morogoro), Nkome (Geita) na Tanga (Songea). Na pia tulisimamisha
Mgombea katika Uchaguzi wa Ubunge Dimani (Zanzibar).
Baada ya kufanya kampeni kubwa mzunguko wa kwanza
tuliweza kutazama na kuamua kuwekeza kwa nguvu kwenye Kata 3.
Pamoja na kuwa hatukushinda Udiwani wala Ubunge
katika Uchaguzi , matokeo yameonyesha kukua kwa kasi kubwa kwa Chama chetu.
Tukishika nafasi ya 2 katika Kata ya Isagehe (Halmashauri ya Mji wa Kahama) kwa
kupata mara 2 ya Kura ya zile ambazo tulipata katika Uchaguzi mkuu wa mwaka
2015, hali hiyo ipo pia katika Kata ya Kijichi jijini Dar es salaam na Nkome mkoani
Geita.
Ni dhahiri kuwa sauti yetu imesikika, Kampeni zetu
zilizojikita juu ya masuala ya wananchi zimeleta matunda kiasi.Nawapongeza sana
viongozi wetu wa Chama katika Jimbo la Kahama Mjini kwa kazi kubwa tulioifanya
na kupiga hatua kubwa. Nawaomba wasikate Tamaa bali wawekeze kwenye kuimarisha
uongozi wa Chama Jimbo zima, kwenye kata zote ili kuwa tayari kwa uchaguzi wa
Serikali za Mitaa.
Katika Kata za Nkome mkoani Geita na Kijichi mkoani
Dar Es salaam tumefanya kazi kubwa Sana. Wagombea na viongozi wetu wa Chama wa
mikoa hii na kata hizi wamepigana kwenye mazingira magumu sana ya ushindani
mkali wa kisiasa. Kata hizi zimetupa fundisho kuwa wananchi wanataka
ushirikiano wa vyama vya upinzani. Ujumbe huo umefika na nawaomba viongozi wetu
wa Chama wajiandae kufanya kazi na vyama vingjne. Ubinafsi, roho mbaya, chuki
na kukomoana hakuwezi kutusaidia. Lazima tubadilike sisi wenyewe kwanza kabla
ya kutaka kuleta mabadiliko kwa wananchi.
Katika Kata ya Tanga Manispaa ya Songea na kata ya
Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro wanachama wetu na viongozi walifanya
kazi kubwa kuonyesha uwepo wa Chama kwenye maeneo yao. Wamepanda mbegu za Chama
na kwa uwezo wa mungu mbegu hizi zitamea na kuzaa matunda.
Ni muhimu kukemea hali ya uchaguzi ya Dimani, Naibu
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano ya Umma – Zanzibar, ndugu Seif Hamad,
ni miongoni mwa waliojeruhiwa kutokana na kipigo baada ya kutolewa Kituoni
alipokuwa Wakala wa Chama kwa kupinga udanganyifu wa uchaguzi. Bado uchaguzi
kwa upande wa Zanzibar hauendeshwi katika misingi ya haki na demokrasia.
Nawapongeza na kuwashukuru sana wanachama wote wa
ACT Wazalendo mliojitoa kwa Hali na Mali kushiriki kampeni katika uchaguzi huu.
Shukran za dhati Kabisa kwa madiwani wetu waliotumia gharama zao kwenda kuishi
vijijini kutafuta kura za Chama chetu. Sina cha kuwalipa mungu atawalipa.
Mmeonyesha mapenzi ya dhati kwa Chama chenu. Mmeonyesha uzalendo wa dhati kwa
vitendo.
Nawapongeza viongozi wa Chama wote wakiwemo wale kwa
Kitaifa kuanzia Mwenyekiti wetu – Mama Anna Elisha Mghwira, Makamu Mwenyekiti –
Mzee Shaaban Mambo, Kaimu Katibu Mkuu – ndugu Said Sanani, na Naibu Katibu Mkuu
– ndugu Msafiri Mtelemwa kwa kazi kubwa walioiafanya. Nawapongeza pia makatibu
wa Kamati za Makao Makuu ya Chama kwa kuwa waratibu wa kata zilizoshiriki
uchaguzi na kwa wale waliokuwa makao makuu kwa kufanya kazi kubwa ya kuwasadia
wenzao waliokuwa kwenye mapambano. Kwa Kweli tumefanya kazi kama timu na sote
tumechangia matokeo haya tuliyoyapata.
Uchaguzi umekwisha. Badala ya kutumia muda wetu
kujadili matokeo, tukubali tumeshindwa na kuanza kujipanga kujenga Chama kwenye
maeneo yetu. Tuwaunge mkono walioshinda lakini pia tuwakosoe wanaposhindwa
kuwajibika. Tusiache kuwasemea wananchi na kuhangaika na changamoto zao za
maisha – msingi wetu wa Siasa zinazojikita juu ya masuala ya wananchi ni muhimu
sana.
Ndio kazi yetu hii Kama Chama cha siasa. Tulitumia
fursa ya kampeni za chaguzi ndogo kupaza sauti kwenye masuala ya kitaifa na
tulifanikiwa Sana kwenye masuala mbalimbali na kutengeneza ajenda za kitaifa.
Tusichoke kuendelea kuwa Chama cha masuala na sio matukio. Chama cha hoja
Badala ya viroja. Chama cha UTU.
Tuendelee kutaka shughuli za kisiasa kuendelea kwa
mujibu wa Sheria. Tuendelee kulaani vikali uamuzi wa Serikali kuzuia vyama vya
siasa kufanya mikutano ya hadhara.
Ahsanteni Sana
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama (KC)
ACT Wazalendo