Zinazobamba

VYUO VIKUU AFRIKA MASHARIKI KUPATA SOMO LA AKILI UNDE


Na Mussa Augustine:Dar es salaam 

Baraza la Vyuo Vikuu Afrika Mashariki (IUCEA) limewakutanisha wataalamu na makamishna wa elimu ya juu kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika warsha maalum ya kuthibitisha na kuridhia somo la msingi la akili unde AI) kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Akizungumza leo Septemba 6,2026 jijini Dar es salaam katika warsha hiyo, Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Vyuo Vikuu Afrika Mashariki( IUCEA) Profesa Idris Rai, amesema lengo la kuandaa somo hilo ni kuhakikisha wanafunzi wote wanaojiunga na vyuo vikuu katika ukanda huo wanapata uelewa wa msingi kuhusu matumizi, fursa na athari za Akili Mnemba.

Profesa Rai amesema akili unde ni teknolojia yenye uwezo wa kusaidia katika kufanya maamuzi, hivyo kuna umuhimu kwa watumiaji kuwa na uelewa wa matumizi yake, pamoja na kuzingatia maadili, usalama na miongozo inayohitajika.

Amesema mpango huo pia unalenga kuwaandaa vijana wa Afrika Mashariki kuwa wabunifu na watengenezaji wa mifumo ya Akili Mnemba inayozingatia maadili, utamaduni na mazingira ya Afrika, badala ya kuwa watumiaji wa teknoloj zinazotengenezwa nje ya ukanda huo.

Amesema somo hilo linapendekezwa kutumika katika programu mbalimbali za elimu ya juu, bila kujali taaluma anayosomea mwanafunzi, ikiwemo Sheria, Tiba, Lugha na Uhandisi, ili kuwawezesha wanafunzi na walimu kutumia teknolojia hiyo kwa ufanisi katika ufundishaji, ujifunzaji na tafiti.Kwa upande wake, Afisa Udhibiti Ubora Mkuu kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Dkt. Mariam Hamisi, amesema TCU inashirikiana kwa karibu na IUCEA katika kuandaa kozi za msingi za akili nde kwa ajili ya elimu ya juu.

Amesema matumizi ya akili unde yamekuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya elimu, huku yakigusa wanafunzi na walimu wa taaluma mbalimbali, ikiwemo Kiswahili, Historia na Udaktari, katika ufundishaji, ujifunzaji na tafiti.

Dkt. Mariam amesema TCU, kupitia jukumu lake la kushauri Serikali, kusimamia na kutoa miongozo kwa vyuo vikuu, itahakikisha matumizi ya Akili Mnemba yanafuata viwango vya ubora, maadili na kulinda hadhi ya taasisi za elimu ya juu.Kwa upande wake, Mhadhiri na Kaimu Mkuu wa Idara ya Sayansi za Kompyuta na uhandisi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Daniel  Ngondya, amesema chuo hicho kinaendelea kushiriki katika kuimarisha matumizi ya akili unde katika elimu pya juu kupitia nafasi yake kama kituo cha AI (AI Node).

Amesema UDOM inashirikiana na vyuo vikuu vingine vya ukanda huo katika kuboresha ufundishaji na tafiti za akili unde huku kuandaliwa kwa kozi maalum kukitarajiwa kuwawezesha wanafunzi kupata uelewa wa matumizi sahihi ya teknolojia hiyo pamoja na misingi ya maadili yake.Naye Mshauri wa Sera za akili unde Afrika Mashariki kutoka Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo la Ujerumani (GIZ), Evelyn Elliseus Rutazala, amesema shirika hilo linashirikiana na IUCEA katika kuvijengea vyuo vikuu na taasisi binafsi uwezo wa kutumia teknolojia hiyo kwa tija.

Amesema lengo ni kuhakikisha Afrika Mashariki haibaki kuwa mtumiaji wa teknolojia zinazotengenezwa na wengine, bali inakuwa na wataalamu wenye ujuzi wa kutengeneza na kutumia akili unde kwa kuzingatia mahitaji ya eneo hilo.

Ameongeza kuwa kujengewa uwezo katika teknolojia hiyo kutasaidia kukuza uchumi na biashara, pamoja na kuongeza uwezo wa Afrika Mashariki kushiriki katika tafiti na ubunifu wa kiteknolojia duniani.

Mpango huo unawezeshwa na Serikali ya Ujerumani kwa kushirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwa lengo la kuimarisha uwezo wa ukanda huo kutumia teknolojia ya akili unde katika elimu, uchumi na maendeleo.

No comments