UHABA WA CHAKULA NCHINI,ZITTO KABWE AIBANA SERIKALI YA MAGUFULI,ASEMA NDIO ILAUMIWE KWA YOTE,SOMA HAPO KUJUA
Wakati Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto
Kabwe akidai kuwa hali ya chakula nchini siyo nzuri kutokana na uhifadhi mbaya,
Serikali imesema hali ni shwari licha ya baadhi ya maeneo kutopata mvua za
wastani.
Zitto alidai jana kuwa Ghala la Taifa la Chakula
(SGR) lina hifadhi ya chakula kinachotosha kwa siku nane tu wakati Novemba 2015
kulikuwa na chakula cha kutosha miezi miwili.
Kwa mujibu wa Zitto, taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) ya Novemba inaonyesha kuwa Mamlaka ya Taifa ya Hifadhi ya Chakula (NFRA),
imebaki na tani 90,476 tu za chakula ambacho amedai ni cha kutosholeza siku
nane.
Hata hivyo, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi,
Dk Charles Tizeba alijibu madai hayo ya Zitto akisema nchi ina chakula cha
kutosha wala siyo cha siku nane wala mwezi pekee, bali zaidi.
Dk Tizeba alisema NFRA inakuwa na akiba ndogo kwa kuwa mwaka 2016 ndiyo ambao nchi ilipata mavuno makubwa ya tani milioni 16 ambazo hazikuwahi kutokea, hivyo maghala ya watu bado yana akiba kubwa ya chakula hivyo wakala haukununua chakula kingi.
Dk Tizeba alisema NFRA inakuwa na akiba ndogo kwa kuwa mwaka 2016 ndiyo ambao nchi ilipata mavuno makubwa ya tani milioni 16 ambazo hazikuwahi kutokea, hivyo maghala ya watu bado yana akiba kubwa ya chakula hivyo wakala haukununua chakula kingi.
“NFRA inanunua chakula kwa kuangalia
mahitaji kwa mwaka huo ukoje, watu wakivuna sana maghala yao yanakuwa yamejaa
na mahitaji ya chakula yanakuwa madogo ndiyo maana Serikali hainunui chakula
kingi. Miaka miwili iliyopita Serikali ilinunua mahindi kwa wingi lakini
yaliishia kuharibika,” alisema Dk Tizeba.
Aliongeza kuwa Serikali sasa ina mradi wa kujenga
ghala jingine lenye uwezo wa kuhifadhi tani 260,000 ili likiungana na la sasa
lenye uwezo wa tani 246,000 nchi iwe na uwezo wa kuhifadhi tani zaidi ya
500,000.
“Kuna maeneo mahindi yameanza kukomaa na
wakulima wa huko watavuna kama kawaida, tunachokifanya tutadhibiti uuzaji wa
chakula nje ya nchi bila vibali ili chakula kisambae zaidi kwa Watanzania. Japo
siwezi kutaja kiasi cha chakula kilichopo kwa sababu za kiusalama, ila
kinatosha siyo kwa siku nane wala mwezi mmoja bali ni zaidi,”
alisema Tizeba.
Juzi wakati akihutubia mkutano wa kampeni za udiwani
katika kata ya Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro, Zitto alisema kauli ya
Rais John Magufuli kwa wananachi wa Mkoa wa Kagera kwamba Serikali haina shamba
ni kuficha uamuzi unaosababisha kukosekana kwa akiba ya chakula ya
kutosha.
Alidai kuwa hali ya chakula nchini si nzuri,
wananchi wanashuhudia namna bei za vyakula zinavyopanda kila siku akidai kuwa
bei ya sembe na mchele zimekuwa juu na gharama za maisha zitaendelea kupanda
kutokana na uhaba wa chakula kuwa mkubwa.
“Hali ya chakula inazidi kuwa
mbaya kwa sababu ya maamuzi mabovu ya Serikali kuhusu hifadhi ya chakula.
Serikali zote zilizopita huko nyuma zilikuwa zinanunua chakula cha akiba ili
wakati wa ukame kama sasa chakula hicho kiingie sokoni, hivyo kushusha bei na
kuwezesha wananchi kumudu gharama za chakula,”
alisema Zitto.
Aliongeza kuwa mpaka sasa NFRA ina tani 90,476 za
chakula wakati kipindi kama hicho mwaka 2015 ghala la chakula lilikuwa na tani
459,561.
Takwimu alizozitoa Zitto Kabwe alizinukuu katika
ripoti ya BoT ya Novemba mwaka jana ambayo inaonyesha kuwa tangu Januari 2016
hadi Julai 2016, akiba ya chakula ilipungua kutoka tani 125,668 hadi 49,632,
lakini hadi Oktoba mwaka huo iliongezeka hadi 90,476.
Ripoti hiyo inaonyesha tofauti ya uhifadhi wa
chakula kwa mwaka jana na miaka mingine miwili iliyotangulia kwani mwaka 2014
Januari, kulikuwa na tani 235,309 na Desemba, tani 466,583 huku mwaka mwaka
2015 Januari kukiwa na tani 459,561 na Desemba 180,746.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Vikundi vya
Wakulima Tanzania (Mviwata), Steven Ruvuga alisema hali halisi kwa wakulima
siyo nzuri kwa kuwa mvua zilinyesha chini ya kiwango, hivyo kuna hofu ya
ukosefu wa chakula cha kutosha baadaye.
“Sasa hivi nipo Kiteto na kwa kawaida
mahindi yalipaswa kuwa tayari yameinuka kufikia walau mabega ya mtu mzima,
lakini nikiyatizama sasa bado yako chini.
"Mwaka huu kuna hatari ya ukosefu
wa chakula na naishukuru Serikali kwa kuwa imeanza kuchukua hatua katika maeneo
yenye uhitaji,” alisema Ruvuga.
Aliongeza kuwa Ghala la Taifa linapaswa kuwa na
wastani wa tani 300,000 za akiba lakini kama sasa zipo 90,476 zinaweza
zisikidhi mahitaji ya kila mtu hivyo ni vyema ikabuni mpango mbadala.