MTEULE WA RAIS MAGUFULI MATATANI,SOMA HAPO KUJUA
| John Magufuli, Rais wa Tanzania (kulia) akiwa na Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam |
MTEULE wa Rais John Magufuli anatajwa kuwa kikwazo
katika ujenzi wa jengo la kitegauchumi lililopo katika Wilaya ya Temeke, jijini
Dar es Salaam, anaandika Dany Tibason.
Ni
Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye amebebeshwa tuhuma hizo leo
katika kikao cha Baraza Kuu kilichofanyika mjini Dodoma.
Tuhuma hizo zimetolewa na Suleiman Kikingo,
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU)-Taifa wakati
akimkaribisha Jenistar Mhagama, Waziri wa Kazi,Vijana na Watu wenye Ulemavu
aliyekuwa ngeni rasmi.
Mbali na tuhuma hizo, chama hicho kimesema Makonda
amekuwa na tabia ya kujifungia ofisini kwake huku hakishindwa kuonana na
viongozi wa chama hicho ili kufanya mazungumzo juu ya uendelezaji wa
kitegauchumi hicho.
Kikingo amesema, serikali inatakiwa kuingilia sakata
hilo ambalo limesababishwa na Makonda kabla taasisi hiyo haijachukua hatua
zaidi.
Amesema Makonda amesimamisha ujenzi huo bila kuwepo
kwa viongozi TALGWU kutoa hoja ya kuangalia ubora wa viwango vya ujenzi.
“Tunaiomba serikali kuhakikisha inaingilia kati
suala hili maana linaonekana kutugawa,wakati wa ujenzi wa jengo letu la
kitegauchumi lililopo Wilaya ya Temeke bila hata kuwepo kwa viongozi huku
akitoa hoja ya ukaguzi wa viwango vya ubora wa jengo.
“Baada ya kupata taarifa hizo tumeweza kuwasilisha
nyaraka zote lakini bado mkuu huyo ameendelea kukaa kimya na tulitegemea jengo
hilo liwe limekamilika kati ya mwezi wa tatu au wa nane mwaka jana.
“Lakini kwa uvivu wa kutekeleza majukumu yake au
chuki binafsi amezidi kukwamisha ujenzi huo na kutokana na hali hiyo, chama
kinajikuta kikiingia katika hasara kutokana na kulipa mkopo ambao unariba
ambayo inatakiwa kutolewa kutokana na kuchelewa kumalizika kwa jengo hilo,”
amesema.
Amesema kuwa, pamoja na juhudi ya kufanya kila mbinu
ya kumaliza jambo hilo, bado Makonda amegoma kukutana na viongozi.
“Amekuwa akitugandisha ofisini kwake toka saa 2
asubuhi hadi saa 12 jioni huku zikitolewa taarifa kuwa hayupo ofisini wakati
yupo.
“Sisi viongozi tumekuwa tukitoka Arusha na mwingine
Mtwara lakini tunapoteza nauli ambayo ni michango ya wanachama,” amesema.
Kwenye mkutano huo Mhagama amesema, jukumu hilo
atalibeba kwa nia ya kutatua ili chama kiweze kupata kitegauchumi chake.
Amesema, kitendo cha kuwepo kwa kitegauchumi ni
jambo jema kwa wanachama na kinaweza kuwaondolea matatizo katika masuala ya
kiuchumi.
“Kama chama kitakuwa na kitegauchumi chake, kitaweza
kupunguza matatizo ambayo wanachama na watumishi wa Umma wanakutana nayo kwa
kunyanyaswa na taasisi za kifedha ambazo zinajifanya kuwasaidia kumbe
zinawakamua,” amesema Mhagama.