MIKATABA 9 YASAINIWA NA SERIKALI YA TANZANIA NA UTURUKI LEO,SOMA HAPO KUJUA
Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Serikali ya Tanzania na Serikali ya Uturuki
zimesaini mikataba tisa ya makubaliano ya kiuchumi inayolenga katika kuimarisha
uhusiano na ushirikiano wa maendeleo baina ya nchi hizo.
Mikataba hiyo inahusisha sekta za uchukuzi,
mawasiliano, habari, elimu, utalii, utafiti, viwanda, afya na ulinzi.
Akizungumza mara baada ya kusaini kwa mikataba
hiyo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Magufuli alisema ujio wa Rais wa Uturuki na ujumbe wake ni
kielelezo cha ukuaji wa mahusiano baina ya Tanzania na Uturuki katika nyanja ya
biashara na kimaendeleo baina nchini hizo.
Rais Magufuli alisema katika mazungumzo yake
aliyofanya na Rais Recep Erdogan kuhusu ujenzi wa Reli ya Standard Gauge
nchini, alimjulisha kiongozi huyo kuwa miongoni mwa wakandarasi walioomba
zabuni ya ujenzi wa reli hiyo kuwa ni kampuni kutoka Uturuki, hivyo endapo
itashinda zabuni hiyo itasaidia kukuza uhusiano uliopo baina ya nchi hizi
mbili.
Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa, Serikali ya
Tanzania inatarajia kuomba mkopo kupitia Benki ya Exim ya Uturuki katika
kujenga sehemu ya kipande cha ujenzi wa reli hiyo.
Rais magufuli alisema Tanzania inaendelea kunufaika
na uwepo wa Shirika la Ndege la Uturuki kwa kufanya safari zake za moja wka
moja kutoka nchini Uturuki, kwa kuwa utasaidia kuongezeka kwa idadi ya watalii
nchini na hivyo kukuza uchumi wa nchi hizo.
Kwa upande wake Rais wa Uturuki, Recep Erdogan
alisema kuwa uwepo wa mikataba hiyo baina ya Tanzania na Uturuki itasaidia
kupata matokeo mazuri ya uhusiano pamoja na fursa mbalimbali za ushirikiano
katika nyanja ya Kilimo, Utalii, Ulinzi, Reli ambazo zitawezesha kukuza uchumi
wa mataifa hayo.
Rais Erdogan alisema kuwa Uturuki imelenga kukuza
ushirikiano uliopo baina yake na Tanzania kupitia makongamano ya
wafanyabiashara yenye malengo ya kukuza uchumi, kuongeza ajira pamoja na kukuza
ujasiriamali baina ya Tanzania na Uturuki.
“Kiwango cha Biashara ya uwekezaji katika nchi ya
Uturuki ni Dola za kimarekani 150 ambapo lengo letu ni kufika Dola za
kimarekani 500,” alisema Rais huyo.
Aidha Rais Erdogan alisisitiza kuwa kufanya kazi kwa
pamoja kutasaidia nchi hizi kusonga mbele na kufanikiwa katika nyanja
mbalimbali.
Nae Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne
Maghembe alisema kuwa makubaliano ya mkataba baina ya Tanzania na Uturuki
katika Sekta ya Utalii yatasaidia katika kutangaza vivutio vilivyopo nchini,
kubadilishana wataalamu, kubadilishana taarifa na kuongeza idadi ya watalii
nchini.
Prof. Magembe aliongeza kuwa makubaliano hayo
yatakuza sekta ya utalii katika kuvutia uwekezaji wa katika maeneo ya hoteli,
fukwe na mbuga za wanyama zilizopo nchini.