ECOWAS: Hakuna makubaliano yoyote ya Jammeh kutoshtakiwa
Viongozi wa nchi za Afrika Magharibi wamesema kuwa,
hakuna makubaliano yoyote ya kutoshtakiwa kwa rais Yahya Jammeh yaliyofikiwa
mwishoni mwa juma, makubaliano yaliyomshawishi kiongozi huyo kuondoka mwenyewe
kwa hiari nchini mwake, amesema waziri wa mambo ya Kigeni wa Senegal.
Jammeh, ambaye anatuhumuwa kwa uvunjifu mkubwa wa
haki za binadamu wakati wa utawala wake, aliliongoza taifa la Gambia kwa miaka
takriban 22, lakini akakataa kukubali matokeo ya uchaguzi mkuu wa Desemba mosi
mwaka jana.
Jammeh aliondoka mjini Banjul siku ya Jumamosi, saa
chache kabla ya vikosi vya ukanda wa ECOWAS kuingia mjini Banjul kudhibiti hali
ya usalama na kuandaa mazingira ya rais Adama Barrow kurejea.
Kuondoka kwa Yahya Jammeh nchini Gambia kunatoa
nafasi sasa kwa rais Barrow kurejea nchini mwake baada ya kuwa amekula kiapo
katika ubalozi wa nchi yake nchini Senegal.
Uamuzi wa Jammeh kuondoka nchini mwake, ulizua
maswali kuhusu makubaliano yaliyofikiwa kati yake na wakuu wa nchi za ECOWAS
katika mazungumzo ya siku mbili mfululizo mwishoni mwa juma, mazungumzo
yaliyoongozwa na rais wa Guinea, Alpha Conde na mwenzake wa Mauritania, Mohamed
Ould Abdel Aziz.
Akizungumza na shirika la habari la Reuters, waziri
wa mambo ya kigeni wa Senegal, Mankeur Ndiaye, amesema kuwa, wakuu wa nchi za
ECOWAS hawakukubaliana chochote kuhusu kutoshtakiwa kwa Jammeh licha ya kufikia
makubaliano.
Waziri Mankeur amesema kuwa Jammeh na timu yake
walikubali kuondoka baada ya kuahidiwa usalama na kupewa hakikisho chini ya
makubaliano yaliyopendekezwa na umoja wa Mataifa, ECOWAS na umoja wa Afrika,
makubaliano ambayo hata hivyo hayakutiwa saini na upande wowote.
Waziri huyu amesema haya baada ya kutolewa kwa
chapisho la makubaliano ya umoja wa Afrika na umoja wa Mataifa kuhusu
mapendekezo ya kufikia suluhu ya amani ya kisiasa nchini Gambia.
Katika hatua nyingine, vikosi vya nchi za ECOWAS
tayari vimewasili mjini Banjul, Gambia, ambako vimeenda kwaajili ya kutoa
usalama kwa rais Barrow na raia wa Gambia.
Chanzo:RFI
Chanzo:RFI