Mbeya: Maiti iliyozikwa yakutwa chumbani kwenye godoro.,
Wakazi wa Isanga Jijini Mbeya wamekumbwa na taharuki
baada ya tukio lisilo la kawaida ambapo maiti iliyokwenda kuzikwa katika
makaburi ya zamani ya Isanga ilikutwa ikiwa kwenye godoro ndani ya nyumba
alimofia.
Taarifa yaJeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya inasema kuwa
tukio lilitokea mnamo tarehe 16.01.2017 majira ya saa 4:30 asubuhi katika mtaa
wa Igoma “A”, Kata ya Isanga, Jijini Mbeya.
Kufuatia taarifa hiyo Polisi walifuatilia na kubaini
kuwa tarehe 16.01.2017 majira ya saa 1:00 asubuhi mtu mmoja aitwaye JAILO
KYANDO na mke wake aitwaye ANNA ELIEZA wote wakazi wa mtaa wa Igoma “A”
waliamka asubuhi na kukuta mtoto wao wa kwanza aitwaye HARUN JAILO KYANDO
amefariki dunia akiwa amelala.
Taarifa za awali zinadai kuwa marehemu tangu utoto
wake alikuwa na matatizo ya ugonjwa wa kifafa hali iliyopelekea kuishi nyumbani
pasipo kusoma.
Kufuatia kifo hicho msiba uliendeshwa na taratibu za
mazishi zilifanyika. Majira ya saa 6:00 mchana jeneza lililetwa msibani na
kuwekwa sebuleni kando ya mwili wa marehemu ambao ulikuwa umeviringishwa na
blanketi na kulazwa chini kwenye godoro, baada ya maombi yaliyoongozwa na
walokole waitwao BONDE LA BARAKA vijana walibeba jeneza hadi makaburi ya zamani
ya Isanga na kisha jeneza kuzikwa.
Waombolezaji waliporudi nyumbani walitaharuki kuona
mwili wa marehemu mtoto HARUN JAILO KYANDO ukiwa chumbani umelazwa eneo
ulipokuwa awali.
Kutokana na hali hiyo taarifa zilifikishwa Polisi
mara moja, askari Polisi walifika na kurejesha hali ya amani kwa kuuchukua mwili
wa marehemu ambao kwa sasa umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya.
Taratibu nyingine za mazishi zitafanyika leo tarehe
17.01.2017. Mpaka sasa bado haijafahamika ni uzembe /bahati mbaya wafiwa
kusahau kuweka mwili wa marehemu kwenye jeneza au kulikuwa na hujuma zozote.
Upelelezi unaendelea kuhusiana na tukio hili.