CHADEMA YAJIPANGA KIVINGINE,NI KUHAKIKISHA WANAMTOA MBUNGE LEMA SERO,SOMA HAPO KUJA
Chadema imeamua kuja na mpango mpya wa kuhakikisha
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema anatolewa mahabusu.
Lema amekuwa mahabusu tangu Novemba mwaka jana,
lakini chama hicho kimesema sasa kinataka apate haki ya kisheria na kuwa huru
kwa kuwatumia wanansheria katika kesi mbalimbali zinazomkabili.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amesema
hayo baada ya yeye, mwenyekiti wake, Freeman Mbowe pamoja na viongozi wengine
kumtembelea Lema mahabusu anakoshikiliwa tangu Novemba 2, mwaka jana kwa tuhuma
za kutoa lugha za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.
Lema amekuwa akikwama kupata dhamana kutokana na
sarakasi za kisheria zilizosababisha upande wa utetezi uende hadi Mahakama Kuu
katika kuhakikisha anapata haki hiyo, lakini hadi sasa bado vita hiyo ya
kisheria haijaisha.
Lissu amewaambia waandishi wa habari mjini Arusha
kwamba wataongeza nguvu ya mawakili wa Chadema katika kesi hiyo kila
itakapokuwa ikitajwa mahakamani.
Pia, watakiandikia Chama cha Wanasheria wa
Tanganyika (TLS) barua rasmi kukitaka kitoe tamko kwa namna yoyote ili kiseme
katika kesi ya Lema kipo upande upi na kama kikisema hakihusiki, basi
hakutakuwa na chama cha wanasheria nchini na wakiona kuna hoja, basi watawataka
watoe mawakili waliopo Arusha kusaidia kesi zinazomkabili Lema.
“Hawa wanasheria wasijidai hamnazo wakati
mbunge wao yupo mahabusu. Tutawaambia wawepo mahakamani kwa kuwa wananchi
wa kawaida hawaruhusiwi kuja kusikiliza kesi hiyo, basi wajae wanasheria,”
amesema Lissu.
Awali, Mbowe amesema chama na viongozi waliamua
kwenda kumuona Lema na familia yake kwa kuwa yupo mahabusu kinyume na haki za
binadamu.
“Lema ana moyo mkuu sana na amejifunza mambo mengi
kwa mujibu wa maelezo yake. Anasema wapo mahabusu asilimia 70 wenye makosa
yanayostahili kupewa dhamana, lakini hawajapewa,” amesema.