ASKOFU MOKIWA AZIDI FIKA BAYA,SASA WAUMINI WAAMUA KUMZUIA KANISANI,SOMA HAPO KUJUA
Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam wa Kanisa la
Anglikana, Dk valentino Mokiwa jana alishindwa kuendesha vikao viwili baada ya
kundi la waumini kufika Usharika wa Ilala kwa lengo la kuzuia.
Askofu Mokiwa, ambaye anapinga uamuzi wa Askofu Mkuu
wa Anglikana, Dk Jacob Chimeledya kumvua madaraka kutokana na tuhuma za
matumizi mabaya ya fedha, alikuwa aendeshe vikao vya kamati ya fedha na
halmashauri kuu, lakini alilazimika kuviahirisha baada ya kundi hilo kufika
eneo hilo.
Wakati waumini hao wakizuia vikao hivyo kufanyika,
mashemasi, mapadri, wainjilisti na waumini wa dayosisi hiyo wametoa tamko la
kumuunga mkono Dk Mokiwa wakipinga uamuzi wa mkuu wa kanisa hilo kumvua
madaraka.
Askofu Mokiwa anapinga uamuzi wa kumvua madaraka
akisema hauwezi kufanywa na mkuu wa kanisa, bali na halmashauri kuu ya jimbo
ambayo anasema haikushirikishwa zaidi ya kutaarifiwa uamuzi huo.
Tukio la jana la kumzuia Dk Mokiwa kufanya mkutano
lilitokea saa mbili asubuhi katika Kanisa la Mtakatifu Nicolau wilayani Ilala,
ambako kuna ofisi ya Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam.
Mmoja wa watu walioshiriki kuzuia vikao hivyo, Haule
Sylvester ambaye alijitambulisha kuwa kiongozi wa waumini wa Anglikana jijini
Dar es Salaam, alisema walichukua uamuzi huo kwa kuwa Dk Mokiwa ameshavuliwa
uaskofu.
“Huyu (Dk Mokiwa) hapaswi kufanya
shughuli zozote za kanisa kwa sababu si askofu. Lakini amekuwa akiendesha vikao
vya siri na mapadri wanaomuunga mkono,” alisema Sylvester.
“Jana (juzi) alifanya kikao cha siri.
Leo (jana) alikuwa aongoze vikao viwili, kikiwamo cha bodi ya fedha ya dayosisi
hii, ndiyo maana tumemzuia.”
Alifafanua kuwa baada ya kikao hicho cha fedha
kilichokuwa kimepangwa kuanza saa 3:00 asubuhi, kikao ambacho kingefuata ni cha
halmashauri kuu ya dayosisi ambacho kingefanya uamuzi wa mambo ambayo
yangejadiliwa na bodi ya fedha.
Sylvester alisema kwa mujibu wa katiba ya dayosisi
hiyo, vikao hivyo vyote vinatakiwa viongozwe na mwenyekiti ambaye ni askofu wa dayosisi.
Alisema halmashauri ina wajumbe 10 akiwamo askofu wa
dayosisi, wakati kikao cha bodi ya fedha kina wajumbe zaidi ya 200 na kina
lengo la kupanga bajeti ya mwaka.
“Ki utaratibu ili kuendesha vikao hivi,
lazima uwe askofu wa jimbo la Dar es Salaam. Tunamsihi Mokiwa aache kufanya
kazi na kutumia ofisi kwa kofia ya uaskofu,” alisema.
Alisema waumini wengi walipanga kushiriki katika
mchakato huo, lakini walienda 20 baada ya kutoa taarifa polisi.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Yohana Sanga ambaye
ni ofisa habari wa Dk Mokiwa alisema vikao hivyo vilikuwa vya kawaida vya
dayosisi hiyo na vililenga kujadili maendeleo ya kanisa.
“Tulishangaa kuona kundi lile la watu,
ambalo chimbuko lake limetoka Kanisa la Magomeni linalompinga Askofu Mokiwa,”
alisema.
Mbali na kundi hilo, kilichowasikitisha zaidi ni
kuona magari sita ya polisi, wakiwamo wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU),
yaliyokuwa yameegeshwa nje ya kanisa.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Ilala, Salum
Hamduni alisema kuwa askari hao walikuwa katika doria ya kawaida.
Sanga alisema baada ya kundi hilo kufika katika eneo
hilo, liliingia moja kwa moja kanisani na walipowauliza walijibiwa kuwa
wanakwenda kujadili masuala ya kanisa.
Alisema baada ya kuona hivyo, walisita kufungua ofisi
iliyoandaliwa kwa ajili ya vikao na baada ya majadiliano ya muda mrefu,
waliahirisha.
“Walivyoona hatufungui ofisi, waliamua
kuondoka kwa mafungu.Lengo lao lilikuwa kuvunja vikao hivi,”
alisema Sanga.
Taarifa ya viongozi hao wanaomuunga mkono Askofu
Mokiwa, inasema bado wanaendelea kumtambua na kumuunga mkono kiongozi huyo kama
askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam na kwamba uamuzi uliochukuliwa dhidi yake
ni batili.
Hivi karibuni, Askofu Mkuu, Chimeledya alimtaka Dk Mokiwa
ajiuzulu kwa kile alichodai kuwa anatumia vibaya madaraka yake na ubadhirifu wa
fedha.
Hata hivyo, Dk Mokiwa alikanusha madai hayo na
kusema mgogoro wa kanisa hilo ni wa kutengenezwa na maadui zake.