ZITTO KABWE AZIDI KIMBIWA CHAMA CHAKE,VIGOGO WAMTOSA,SOMA HAPO KUJUA
Aliyekuwa Katibu wa Bunge na Serikali za Mitaa katika
Sekretarieti ya Chama cha ACT-Wazalendo, Habibu Mchange, amejiondoa uanachama
wa chama hicho na kujiweka kando na siasa.
Taarifa ya uamuzi huo wa Mchange ilisambazwa jana
katika mitandao ya kijamii, ikionyesha kuandikwa naye huku ikiambatanishwa na
namba yake ya simu.
Katika andiko hilo, Mchange aliyewahi kuwa
mwanachama wa Chadema kabla hajahamia ACT Wazalendo, alisema aliamua kujitoa
rasmi katika ushiriki wa aina yoyote ya siasa ili apate muda zaidi wa kusimamia
shughuli zake za kijasiriamali.
Mchange alisema ameamua kujiengua na siasa ili kutoa
fursa na huduma sawa kwa viongozi na wanachama wa vyama vyote vya siasa.
“Kwa moyo mkunjufu kabisa na kwa mapenzi mema na
taifa langu, ninathibitisha kwamba nimejitoa rasmi katika ushiriki wa aina yote
ya siasa ili nipate muda mwingi zaidi kufanya na kusimamia shughuli zangu za
kijasiriamali zinazonitaka nitoe fursa na huduma sawa kwa viongozi na wanachama
wa vyama vyote vya siasa,” alisema Mchange.
Alisema kutokana na uamuzi huo ambao aliomba uheshimiwe,
lolote atakalolifanya lisihusishwe na chama bali iwe ni msimamo wake mwenyewe
kama mtu huru asiye na chama.
“Ninafahamu kuwa mwanachama wa chama cha siasa ni
haki yangu ya kikatiba, lakini nimeamua kuihifadhi kwa sasa mpaka hapo
nitakapoona inafaa kufanya vinginevyo. Ninawatakia kila la heri waliokuwa
wanachama wenzangu wa ACT Wazalendo katika kuyafikia malengo ya msingi ya
uanzishwaji wa chama hicho,” alisema Mchange.
Mchange alisema kujiondoa kwake kusihesabiwe kama
sehemu ya kukwamisha au kurudisha nyuma matarajio na au malengo ya chama hicho
bali ichukuliwe kama chachu ya kufika mbali.
“Msivunjike moyo, msirumbane, pendaneni,
heshimianeni na shikamaneni ili mfikie lengo. Nitabaki na kuendelea kuwa ndugu
yenu, rafiki na swahiba. Zaidi Mtanzania mwenzenu. Tutaendelea kushirikiana
katika mambo yote ya kijamii na kimaisha yasiyohusiana na mlengo wa kiitikadi
wa kisiasa,” alisema Mchange.
Mchange alishika nafasi mbalimbali katika chama
hicho ikiwamo Katibu wa Mipango na Mikakati, Mjumbe wa Kamati Kuu, Mjumbe wa
Halmashauri Kuu na Mjumbe wa Mkutano Mkuu.
Mchange anakuwa mwanasiasa wa tatu kuondoka
ACT-Wazalendo mwaka huu baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Samson
Mwigamba kuachia nafasi yake na kwenda masomoni nchini Kenya, Aprili mwaka huu.
Miezi michache baadaye, Novemba mwaka huu mwanasiasa
Moses Machali naye alitangaza kujiondoa rasmi chama hicho na kuunga mkono
jitihada zinazofanywa na Rais Dk. John Magufuli.
Machali aliwahi kuwa Mbunge wa Kasulu Mjini kupitia
Chama cha NCCR-Mageuzi kabla ya mwaka jana kushindwa kutetea jimbo lake kupitia
ACT-Wazalendo.