Zinazobamba

MWAKIPOSA AWA MWENYEKITI MPYA WA WENYEVITI WA SERIKALI ZA MITAA MKOA WA DAR ES SALAAM


Mwenyekiti wa Wenyeviti Mkoa wa Dar es salaam Razalous Mwakiposa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutangazwa mshindi wa nafasi hiyo.

Na Mussa Augustine

Uchaguzi wa nafasi za Mwenyekiti na Katibu Mkuu wa Umoja wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Dar es Salaam umemalizika leo, Juni 20, 2026, huku mgombea Razalous Mwakiposa akishinda nafasi ya Mwenyekiti na Peppino Sudi Peppino akishinda nafasi ya Katibu Mkuu.

Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi huo, msimamizi wa uchaguzi, Bw. Kambi Sinde, amesema kuwa Razalous Mwakiposa ameshinda kwa kupata kura 24 kati ya kura 37 zilizopigwa, huku Katibu Mkuu akishinda kwa kura 20 kati ya kura 37 zilizopigwa."Uchaguzi umefanyika kwa uwazi na haki. Kulikuwa na jumla ya wajumbe 40, lakini watatu walipata udhuru. Hivyo, leo waliopiga kura ni wajumbe 37 na matokeo ni kwamba mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti amepata kura 24 kati ya kura 37 zilizopigwa, huku Katibu Mkuu akipata kura 20 kati ya kura 37 zilizopigwa," amesema Sinde.

Sinde amefafanua kuwa wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti walikuwa watatu ambao ni Consolatha Modest Rwiza aliyepata kura 11, Juma Abas Mwingamno aliyepata kura 2, na Razalous Anosisye Mwakiposa aliyeibuka mshindi kwa kura 24.

Kwa upande wa nafasi ya Katibu Mkuu, wagombea walikuwa wawili ambao ni Athumani S. Gereza aliyepata kura 17 na Peppino Sudi Peppino aliyeshinda kwa kura 20.Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya uchaguzi huo, Mwenyekiti mpya wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Dar es Salaam, Razalous Mwakiposa, ameushukuru umoja huo kwa kumchagua kuwa kiongozi wao na kusema kuwa, pamoja na mambo mengine, atahakikisha anapigania maslahi ya wenyeviti wa serikali za mitaa ili waweze kulipwa posho au mishahara inayokidhi mahitaji yao.

"Sisi ndio tunatumia muda mwingi ofisini kuwahudumia wananchi. Tunamuomba Mama (Rais Dkt. Samia) atukumbuke watoto wake tulipwe posho ama mshahara unaoweza kutusaidia kukidhi mahitaji yetu ili tufanye kazi kwa ufanisi mkubwa," amesema Mwakiposa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Boko, Wilaya ya Kinondoni.

Akizungumzia suala la ulinzi na usalama, Mwakiposa amesema kuwa atashirikiana na wenyeviti wenzake kuhakikisha kunakuwepo vikundi vya ulinzi shirikishi katika kila mtaa, hali ambayo italeta utulivu na kuondoa vitendo vya uhalifu mkoani humo.Katibu Mkuu Peppino Sudi Peppino akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutangazwa mshindi wa nafasi hiyo.

Naye Katibu Mkuu wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Dar es Salaam, Peppino Sudi Peppino, amesema kuwa yeye kama Mtendaji Mkuu wa umoja huo atashirikiana na mwenyekiti pamoja na wenyeviti wengine kufikia malengo waliyojiwekea.

Picha tofauti Mwenyekiti wa Wenyeviti Mkoa wa Dar es salaam Razalous Mwakiposa akiwashukuru wajumbe waliopiga kura na kumpitisha kua Kiongozi wao ngazi ya Mkoa.


No comments