MCHUNGAJI LUSEKELO AIBUKA NA HIKI LEO,SOMA HAPO KUJUA
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony
Lusekelo, maarufu kwa jina la Mzee wa Upako jana amesema waandishi wote wa
habari wanaoandika habari za kumchafua, watakufa kabla ya kufika Machi 2017.
Kauli hiyo ameitoa ikiwa ni mwendelezo wa mahubiri
yake ya nne katika wiki ya tatu mfululizo, akijibu yale yaliyoandikwa katika
vyombo vya habari kuhusu kumfanyia fujo jirani yake na kulewa.
“Kila mwandishi aliyeniandika vibaya, ikifika
mwezi wa tatu akiwa hai, mimi naacha kuhubiri, nafunga virago nakwenda kuuza
gongo, sasa Mungu ndiye ataamua kwamba ama niache kuhubiri mimi au wewe ufe
…najua hata leo mko humu mmekuja na mnasikiliza tu,”
alisema.
“Akisema Mungu uishi wewe basi, nakuwa
sina namna, lakini sijawahi kumtumikia Mungu ambaye ananyamaza.
Nilishakubaliana mimi na Mungu, mpango wa Mungu ndiyo mpango wangu, sasa
wajiandae, mimi siyo Sheikh Yahaya, mmeingia choo cha kike, nasema ‘Mama yangu
mzazi’ nitaacha kuhubiri, nitaacha kuhubiri ….mimi nina nguvu saaana,”alisema.
Hata hivyo baadaye mchungaji huo alishuka na kusema
anamuachia Mungu wake ambaye atawahukumu kwa wakati wake.
“Lakini Mungu anasema tusihukumu,
namuachia Mungu atawahukumu kwa wakati wake, haleluya, haleluya, Mungu
awabariki sana."
Novemba 24, mitandao ya kijamii ilikuwa na picha
zinazomuonyesha Mzee wa Upako akirushiana maneno makali na jirani huyo ambaye
anasikika sauti.
Taarifa za kukamatwa kwa kiongozi huyo wa kiroho
zilisambaa baada ya mwandishi wa habari, Happiness Katabazi aliyeshuhudia tukio
hilo, kuandika kwa urefu kisa hicho na kusambaza kwenye mitandao ya kijamii.
Novemba 26, Mzee wa Upako kwa mara ya kwanza alisita
kuzungumzia sakata hilo na badala yake akasema wanaomtuhumu waendelee kusema:
“Sisemi, lakini siogopi kwenda jela mimi na kwa taarifa yao watashindana sana,
lakini hawatashinda. Hii ni kama kumpiga chura teke.”
Novemba 28, pia Mchungaji huyo akajibu akisema
maneno aliyotumia ambayo ni mshenzi, mpumbavu na mjinga siyo matusi kwani
yameandikwa kwenye biblia na kwamba watu hao ndiyo walianza kumtukana yeye
baada ya kuwauliza wanatafuta nini eneo la getini kwake.
Jana, mchungaji huyo aliwahakikishia waumini wake
akisema waandishi walioandika kwa lengo la kumchafua watakufa kabla ya kufika
Machi mwakani.
Katika mahubiri yake yaliyojengwa na msingi wa
Biblia kutoka kitabu cha Samweli wa kwanza, sura ya 16, mstari wa saba, Mzee wa
Upako aliyekaribishwa kwa nyimbo kadhaa ikiwamo ‘kusanya kusanya’ alisema yeye
siyo mchungaji anayejikweza, lakini baadhi ya wachungaji wakubwa kutoka nje
wamekuwa wakienda kuomba upako.
Pia, alisema hata Rais John Magufuli hakumuita yeye
bali aliona kitu ndani yake na kubarikiwa kabla ya kumtembelea.