MAALIM SEIF AISHUTUKIA FITINA YA NEC,SOMA HAPO KUJUA
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema
uamuzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wa kutaka pande zinazovutana ndani ya
chama hicho kuteua kwa pamoja jina la mgombea ubunge katika uchaguzi mdogo wa
Jimbo la Dimani kuwa ni wa kukurupuka.
Desemba 8, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhani
Kailima alisema fomu za wagombea wa CUF katika uchaguzi huo zitapaswa kusainiwa
na pande mbili zilizo na mgogoro wa uongozi.
“Kipengele cha 4 (5) (iii) cha Sheria ya
Uchaguzi kinataka fomu za wagombea kwenye chama chenye mgogoro zisainiwe na
viongozi wakuu wote wawili kwa vile wamethibitishwa na Msajili wa Vyama Siasa,”
alinukuliwa
Kailima.
Lakini juzi, Maalim Seif alizungumzia uamuzi huo wa
NEC na kusema kila chama cha siasa kina kanuni na taratibu zake za kuwapata
wagombea wa nafasi mbalimbali.
“NEC wamenishangaza kwa sababu nchi
inaendeshwa kwa sheria na kanuni labda nimuulize Kailima ameitazama Katiba ya
CUF inasema nini kuhusu mchakato wa wagombea? Tume inatoa uamuzi wa kisiasa
ambao haukupaswa kutolewa na chombo hiki muhimu,” alisema
Maalim Seif.
Hata hivyo, licha ya kushangazwa na hatua hiyo,
Maalim Seif hakuwa tayari kutoa msimamo wa CUF juu ya suala hilo akisema: “Ni
mapema mno kusema tutafanya nini?”
Tayari Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor
Ahmed Mazrui amesema lengo la NEC ni kutaka chama hicho kikose mgombea.
Wakati Maalim Seif akieleza hayo, Mwenyekiti wa CUF,
Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa
alisema:
“Tutaweka utaratibu na watu wajitokeze
ili tuweze kufanya uteuzi wa mgombea. Ingawa kulikuwa na mgombea wa mwaka jana,
nina imani watajitokeza wengine na Baraza Kuu ndilo litamteua.”
Alisema uchaguzi kwa ngazi udiwani hakuna tatizo kwa
sababu mchakato wake unaishia wilayani, lakini kwa ubunge lazima wakae pamoja.
CUF imekuwa katika mgogoro baada ya Profesa Lipumba
aliyejiuzulu uenyekiti mwaka jana kuibuka na kutaka kurejea kwenye nafasi hiyo,
lakini viongozi wengine wakamuwekea ngumu na kuibua mgogoro uliopo mahakamani.