WAZIRI SIMBACHAWENE AANZA KUWAKOLOMEA WAMACHINGA,SOMA HAPO KUJUA
Waziri wa TAMISEMI George Simbachawene amewataka
wamachinga kutotafsiri vibaya agizo la Rais Magufuli kuwa halikumaanisha
wafanye biashara kiholela mahala popote bila utaratibu bali wazingatie sheria
zilizopo zikiwamo za mipango miji na usafi.
Simbachawene pia amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya
pamoja na mamlaka za serikali za mitaa, kuhakikisha wanatekeleza agizo la Rais
John Magufuli la kuwatafutia maeneo ya kufanyia biashara wafanyabiashara hao na
kuwashirikisha kwenye mchakato mzima wa kubaini maeneo yenye wateja na
miundombinu rafiki.
Aidha, watendaji nao wametakiwa kutotumia tafsiri
hiyo kususa na kuwaacha wamachinga wafanye biashara zao kiholela.
Amesema endapo utaratibu huo utafuatwa pamoja na
mambo mengine utaweza kurasimisha shughuli za wamachinga hali itakayosaidia pia
kundi hilo kuchangia mapato ya halmashauri kwa kiasi kikubwa na kuondoa kabisa
tabia ya kufukuzana fukuzana kila kukicha.