WAZIRI MKUU AFUNGUKIA POLISI,SOMA HAPO KUJUA
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amepiga marufuku watu
binafsi wenye uwezo kifedha kutumia Jeshi la Polisi kuwapiga mabomu na
kuwanyanyasa wananchi kwa kuwapiga mabomu wananchi wasio na silaha.
Ameagiza nguvu hizo wazitumie kwenye maeneo ambayo
yanahatarisha usalama wa nchi na wananchi.
Aidha amewaambia wananchi wa Kata ya Bwawani
Kitongoji cha Omapinu kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
William Lukuvi atafika kijijini hapo wiki ijayo, kuzungumza nao namna ya
kutatua mgogoro wa shamba la Tanzania Plantation na wananchi hao.
Waziri Mkuu Majaliwa aliyasema hayo baada ya
kusimamishwa na wananchi wa kitongoji hicho, wakati alipokuwa akiendelea na
ziara yake mkoani Arusha jana.
“Kuanzia sasa ni marufuku kwa watu
binafsi wenye uwezo wa fedha kutumia Jeshi la Polisi kuwapiga mabomu na
kuwanyanyasa wananchi kwa kuwapiga mabomu wakati hawana silaha.
“Polisi wanaruhusiwa kutumia nguvu hizo
kwenye maeneo ambayo yanahatarisha usalama wa nchi na wananchi na si
vinginevyo,” alisema Waziri Mkuu.
Kuhusu mgogoro wa shamba la Tanzania Plantation,
Waziri Mkuu alihoji; “Ni kwanini polisi wawapige mabomu wananchi wanaozuiwa
kulima au kuchota maji katika eneo hilo la shamba hadi kufikia hatua ya
wanawake kuharibu mimba?
“Nyie polisi kwanini mnawapiga mabomu
hawa watu, nani anatoa amri ya kupigwa mabomu wananchi hawa. Nasema kuanzia leo
msiwapige mabomu watu hawa na pia nawasihi nyie wananchi msifanye fujo,
subirini Waziri Lukuvi anakuja wiki ijayo kwa ajili ya kutatua mgogoro huu wa
shamba.”
Alisema polisi wanaruhusiwa kutumia nguvu, pale tu
panapotokea jambo linaloweza kuhatarisha maisha au vurugu, ila si kuwanyanyasa
wananchi wanaodai ardhi yao kwa kuwapiga mabomu.
Alisema Lukuvi atafika mkoani humo kwa ajili ya
kushughulikia migogoro ya ardhi, ambayo ipo zaidi wilayani Arumeru, na atakaa
muda mwingi kwa ajili ya kutatua kero za wananchi.
Alisema kuanzia sasa mwekezaji ambaye ana mashamba
wilayani humo na hayaendelezi, mashamba hayo yatachukuliwa na serikali ili
kugawanywa kwa wananchi.
Alisema Waziri Lukuvi akiwa wilayani humo pamoja na
kushughulikia migogoro mingine, pia atatatua mgogoro huo baina ya shamba la
Tanzania Plantation na wanachi hao.
Awali, Ofisa Ardhi Wilaya ya Arumeru, Rehema Jato
alikiri kuwepo kwa mgogoro wa ardhi kati ya mwekezaji wa wa Shamba la Tanzana
Plantation, Pradeep Lodhia na wananchi.
Alisema kuna kesi mahakamani na wanachosubiri sasa
ni uamuzi wa Mahakama ndipo hatua zingine zichukuliwe.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti alisema
wilaya hiyo ni moja ya wilaya nchini zenye migogoro mingi ya ardhi na wakati
mwingine watu wanauana.