CCM YASHINDA UCHAGUZI WA MEYA KIGAMBONI,SOMA HAPO KUJUA
Uchaguzi wa kumpata Meya wa Manispaa ya
Kigamboni jijini Dar es Salaam, umefanyika na hatimaye Diwani wa Kata ya Pemba
Mnazi kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), Maabadi Hoja amechaguliwa kuwa Meya wa
kwanza.
Uchaguzi huo ulifanyika jana kwenye ukumbi wa Chuo
Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kigamboni, Rahel Mhando,
ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi, alisema mgombea huyo wa CCM ndiye
aliyeshinda.
Washiriki wengine walitoka vyama vya CCM, Chama cha
Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Mhando alisema
Hoja alipata kura tisa dhidi ya Celestine Maufi (CUF) aliyepata kura tano na
kura moja iliharibika.
Pia, Mhando alisema katika uchaguzi huo, Amini Sambo
ambaye ni Diwani wa Kata ya Kibada, pia kutoka CCM, alishinda nafasi ya Naibu
Meya, akipata kura 10 dhidi ya Ernest Mafimbo wa CUF, aliyepata kura tano.
“Tunashukuru uchaguzi umefanyika vizuri Kigamboni, sasa tumepata Meya na Naibu
Meya,” alisema Mhando.
Uchaguzi wa Meya na Naibu wake kwa upande wa
Kigamboni, umefanywa baada ya Wilaya ya Temeke kugawanywa na kuwa wilaya mbili
za Temeke na Kigamboni.
Mhando alieleza kuwa uchaguzi huo ambao ni wa mara
ya kwanza kwa halmashauri hiyo, ulifanyika kwa amani bila kuwapo na malalamiko.