UFAFANUZI KUHUSU TAARIFA ZA KUKAMATWA KWA WATANZANIA WANAODAIWA NI MAJASUSI NCHINI MALAWI,SOMA HAPO KUJUA
Baadhi ya Vyombo vya habari vya hapa nchini hivi
karibuni vilitoa taarifa kuwa, Watanzania 8 wanaodaiwa kuwa ni majasusi wa
Serikali ya Tanzania wamekamatwa nchini Malawi kwa tuhuma za kuingia kwenye mgodi
wa urani wa Kayerekera uliopo nchini Malawi kinyume cha sheria.
Taarifa hiyo kwa mara ya kwanza ilitolewa na chombo
cha habari cha Malawi ambacho kilidai kuwa watu hao wametumwa na Serikali ya
Tanzania ili kuchunguza kama Serikali ya Malawi inatengeneza silaha za nyuklia
kwa kutumia madini ya urani ya kutoka mgodi huo.
Kufuatia taarifa hizo, Wizara kupitia Ubalozi wa
Tanzania nchini Malawi ulifuatilia ili kubaini ukweli wa tukio hilo. Baada ya
kufuatilia ilibainika kuwa ni kweli Watanzania 8 kutoka taasisi ya CARTAS iliyo
chini ya Kanisa Katoliki Songea mkoani Ruvuma walikamatwa na vyombo vya usalama
katika Wilaya ya Karonga ambayo inapakana na Wilaya ya Kyela.
Watanzania hao mara moja walifunguliwa kesi kwa
kutuhumiwa kufanya kosa la jinai la kuingia eneo la mgodi bila kibali (criminal
trespass).
Ubalozi uliwasiliana na Taasisi ya CARTAS kutaka
kufahamu madhumuni ya watu hao kufanya ziara nchini Malawi. Ubalozi ulielezwa
kuwa ziara hiyo ilikuwa ni ya mafunzo ambapo walitaka kufahamu juu ya madhara
yatokanayo na machimbo ya madini ya urani. Watanzania hao kwa sasa wapo katika
gereza kuu la Mzuzu hadi kesi yao itakapotajwa tena tarehe 04 Januari 2017.
Ubalozi unaendelea kufanya mawasiliano na Kanisa Katoliki
Songea ili kupata maelezo zaidi kuhusu ziara ya watu hao kwa madhumuni ya
kuyawasilisha mamlaka husika ili watuhumiwa waweze kutolewa.
Aidha, Wizara kupitia Ubalozi umebaini kuwa CARTAS
iliruhusu watu hao kufanya ziara nchini Malawi bila kupata kibali kutoka
mamlaka husika na bila kutoa taarifa Ofisi ya Ubalozi kuhusu ziara hiyo.
Aidha, kipindi cha kufanya ziara hiyo nchini Malawi
hakikuwa muafaka kwa kuwa watumishi wa Serikali ya Malawi wanakuwa katika
likizo ya mwaka kuanzia tarehe 22 Desemba hadi 03 Januari 2017. Hii inakwamisha
juhudi za kuwafuatilia watu hao ikiwa ni pamoja na kukwama kwa maombi ya kibali
cha kuwatembelea watu hao tarehe 28 Desemba 2016.
Wizara inatoa wito kwa mara nyingine kwa taasisi za
dini, vyuo vya elimu na watu binafsi kuomba vibali na kufuata sheria za nchi
nyingine wanapofanya ziara za mafunzo au ziara nyinginezo ikiwa ni pamoja na
kuwasiliana na ofisi za Balozi zetu kwa madhumuni ya kufahamishwa taratibu
zinazotakiwa kufuatwa kabla ya kufanya ziara husika ili kuepuka usumbufu
unaoweza kujitokeza.
Wizara, kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi
unaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa suala hilo linapatiwa ufumbuzi kwa
haraka.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 29 Desemba 2016.