MUFTI ZANZIBAR, TIF WAKEMEA MTUME KUVUNJIWA HESHMA
Kufuatia tukio la mkazi mmoja wa Zanzibar aliyejulikana kama Abdallah Saleh la kutoa matamshi ya kumkufuru Allah na kumtusi Mtume wake Muhammad (rehema na amani ya Allah zimfikie), viongozi mbalimbali wa dini wamekemea vikali kitendo hicho na kuishauri serikali kumchukulia hatua zinazostahili ili liwe fundisho kwa watu wengine.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mufti wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi, amesema kitendo kilichofanywa na Saleh kimeumiza hisia za watu wengi na kwamba yeye kama kiongozi mkuu wa Waislamu amesikitishwa sana na anakemea vikali.
Mufti alisema amestushwa na matamshi yaliyotolewa na kijana huyo ambayo kisharia yanapelekea kumtoa mtu katika imani ya Kiislamu pamoja na kuhatarisha amani ya nchi na kuvuruga uhusiano wa Zanzibar kimataifa.
Aliongeza kuwa maneno ya dharau kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na matamshi ya kumvunjia heshima Mtume Muhammad (rehema na amani ya Allah iwe juu yake) pamoja na Waislamu wote kwa ujumla hayapaswi kupuuzwa, yanapaswa kuchukuliwa hatua zinazostahili.
“Linalonisikitisha zaidi ni kule kuona matamshi hayo mazito yametolewa na kijana wa Kizanzibar aliyetokana na mifupa ya Waislamu. Nivyoamini mimi hata Wasiokuwa Waislamu wasingeweza kutamka matamshi kama hayo,” alisema Mufti Kaabi.
Mufti Kaabi amemtaka kijana Saleh kurudi katika Uislamu, amtake msamaha Allah na atubu kwa Mwenyezi Mungu kwa toba ya majuto haraka iwezekanavyo na aazimie katika moyo wake kutorejea tena makosa hayo.
“Nikiwa Mufti Mkuu wa Zanzibar, namtaka Kijana Saleh atubu Kwa Mwenyezi Mungu toba ya majuto kwani jambo ambalo amelifanya ni hatari kwani linaweza kuhatarisha amani ya nchi.”
Aidha, Mufti Kaabi ametoa onyo kwa Waaumini wote kuacha kutamka maneno kama hayo kwa kuendekeza matamanio ya nafsi zao kwani wakifanya hivyo wanaweza kupata laana kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Muhammad (rehema na amani ya Allah iwe juu yake) kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur’an kupitia Surat Ahzaab aya ya 57 na Suratul Tawba aya ya 65-66.
“Natoa onyo kwa Waumini wote kutotamka maneno kama haya kwa kuendekeza nafsi na kufikia kumtusi Mtume wetu Muhammadi (rehema na amani ya Allah iwe juu yake) na kutoka kwenye Twaa ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, wakumbuke kufanya hivyo kunapelekea kupata laana kubwa kutoka kwa Mwezi Mungu.”
Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) Aref Nahdi ameiomba Serikali kutoa adhabu itakayotoa fundisho kwa kijana huyo kwani jambo alilolifanya ni hatari na linaloumiza hisia.
Nahdi alisema: “Matamshi ya dharau dhidi ya Mtume Muhammad (rehema na amani ya Allah iwe juu yake) hayakubaliki. Waislamu tumechukizwa na kitendo lakini tuna imani kubwa na serikali yetu kuwa itachukua hatua sahihi ili iwe onyo na fundisho kwa wengine, wasifikirie wala kuwaza kuifanyia mzaha dini.”
“Matamshi ya kumkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume Muhammad (rehema na amani ya Allah iwe juu yake) yaliyotolewa na Abdallah Saleh ni mabaya sana na kwa nchi nyingine adhabu yake ni kubwa mno.”
Nahdi alisema kuchukizwa kwa Waislamu siyo tu kwa sababu kafanyiwa Mtume Muhammad, bali Waislamu wangeumia iwapo Mtume yoyote angevunjiwa heshima kwani kuamini Mitume ni nguzo miongoni mwa nguzo za imani.
“Tunaiomba Serikali itoe adhabu anayostahili kwani suala hilo likiachwa lipite watu wengine wataibuka na kuwatusi tena Mitume, tena siyo Muhammad peke yake bali Mitume wengine pia,” alisema Nahdi alisema.