TAARIFA MPYA KUHUSU AJIRA ZA WALIMU
Wizara
ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi imesema haihusiki na utoaji wa
ajira za walimu nchini, isipokuwa inachokifanya ni uhakiki wa taarifa za
walimu wenye sifa za kuajiriwa serikalini.
Akizungumza
nakituo cha EATV leo, Naibu Waziri wa Elimu, Mhandisi Stella Manyanya
amesema kuwa kwa sasa wizara hiyo inapitia taarifa (CV) za walimu
waliohitimu ngazi ya Shahada na Stashahada, na baada ya hapo itazituma
taarifa hizo katika Wizara ya Utumishi ambao ndiyo wanaohusika na
kuajiri.
Akizungumzia sababu za kuwatenga wahitimu wa ngazi ya cheti, Manyanya amesema uhitaji mkubwa uliopo kwa sasa ni kwa walimu wa sekondari hususani wa masomo ya Phisics, Hisabati, Chemistry na Biolojia,
hivyo inawahitaji kwa haraka zaidi walimu hao huku akisema wahitimu
wengine ambao siyo wa masomo hayo na ambao siyo kwa ajili ya kufundisha
sekondari, wasubiri utaratibu wa wizara inayohusika na utumishi.
"Siyo
kwamba hatuhitaji walimu wa shule za msingi, lakini uhitaji mkubwa
tulionao kwa sasa ni walimu wa sekondari, sisi hatuajiri, sisi tunafanya
uhakiki, na sasa tunapitia CV za wahitimu waliotuma taarifa zao,
tukishajiridhisha na wale ambao taarifa zao ni sahihi na wana sifa
tunazohitaji, tunazipeleka Utumishi, hao ndiyo wataajiri, halafu majina
yatapelekwa TAMISEMI kwa ajili ya kupangiwa maeneo ya kazi" Amesema Manyanya
Kuhusu
idadi ya walimu wanaohitajika haraka, Manyanya amesema, wanahitajika
walimu wengi kuliko idadi waliyoitoa mwanzo, na kuwataka wote waliotuma
taarifa zao wawe na subira kwa kuwa mchako wa uhakiki bado unaendelea na
majina yatatangazwa muda mfupi ujao ambao hautazidi kipindi cha miezi
mitatu.