SERIKALI YA KOREA YAIPIGA JEKI SERIKALI YA TANZANIA,YATOA DOLA ELFU 50 KWA WAHANGA WA KAGERA,SOMA HAPO KUJUA
Serikali ya Jamhuri ya Korea imetoa msaada wa Dola
za Marekani elf 50,000 takribani milioni 108 kwa fedha za Tanzania kwa ajili ya
waathirika wa tetemeko la ardhi lilitokea mkoani Kagera mwezi Septemba 2016.
Msaada huo ulikabidhiwa leo jijini Dar es Salaam na
Balozi wa Korea nchini Tanzania, Mhe. Song Geum Young na kupokelewa na Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (Mb)
kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim
Majaliwa (Mb).
Baada ya kupokea msaada huo, Dkt. Mahiga aliishukuru
Serikali ya Korea na kuahidi kuwa msaada huo ataukabidhi kwa Mhe. Waziri Mkuu
ili uweze kutumika kama ulivyokusudiwa.
Mhe. Mahiga alisema kuwa Korea imekuwa mbia mkubwa
wa Tanzania tokea nchi hiyo ilipoanzisha mahusiano ya kidiplomasia na Tanznaia
miaka 25 iliyopita. Alieleza kuwa katika kipindi hicho Tanzania imekuwa
ikipokea misaada mbalimbali ya kiuchumi, kijamii na ya kibinadamu ukiwemo huu
wa leo ulioelekezwa kwa waathirika wa tetemeko la ardhi la mkoani Kagera.
Mhe. Waziri alitaja misaada ambayo Korea imeipatia
Tanzania ni pamoja na ujenzi wa daraja la Malagarasi mkoani Kigoma, ujenzi wa
hospitali ya kisasa ya Mloganzila na ujenzi wa hospitali ya uchunguzi wa afya
ya Mama iliyopo Chanika. Aidha, Korea hivi karibuni itaanza ujenzi wa daraja la
Selander ambalo linatarajiwa kuanzia ufukwe wa Coco, Oysterbay hadi maeneo ya
hospitali ya Aga Khan, Upanga jijini Dar es Salaam.
Waziri Mahiga alibainisha pia kuwa Jamhuri ya Korea
itatoa msaada mkubwa zaidi wa maendeleo kwa Tanzania kuliko nchi yeyote ya
Afrika. Taarifa hiyo ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea, Mhe. Yun
Byung-se alipofanya naye mazungumzo kando ya Mkutano wa nchi za Afrika na Korea
uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia tarehe 06 na 07 Desemba 2016.
Kwa upande wake, Balozi wa Korea nchini aliahidi
kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania hususan kutoa atia misaada
ya maendeleo ili iweze kutimiza azima ya Serikali ya awamu ya tano ya kuifanya
Tanzania kuwa nchi ya viwanda.