SAKATA LA KUPOTEA MZUNGUKO WA FEDHA MITAANI,ZAIBUKA NA SURA MPYA,MSAJILI WA HAZINA NAYE ASEMA YAKE,SOMA HAPO KUJUA
Msajili wa Hazina nchini, Lawrence Mafuru
amesema benki nchini zinashindwa kueleza ukweli juu ya kuyumba kwao na kwamba
madai ya kuwa hali zao ni mbaya kutokana na agizo la serikali la kutaka fedha
zake zitunzwe Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hazina ukweli.
Mafuru amesema taarifa ambazo serikali wanazo ni
kwamba benki hizo zaidi ya 50 zimekopesha fedha nyingi kwa watu mbalimbali,
lakini marejesho ya madeni hayo yamekwama kiasi cha kusababisha benki hizo ziwe
katika hali hiyo.
Akizungumza jana Dar es Salaam, Msajili wa Hazina
licha ya kukiri kuwa mzunguko wa fedha umepungua kutokana na Tanzania kuchagua
kwamba fedha inazozipata zitumike katika miradi ya maendeleo badala ya matumizi
ya kawaida, benki zinazolalamika zimeshindwa kurejesha fedha ilizokopesha watu
na taasisi mbalimbali.
Akizungumzia taarifa zinazoenezwa kwamba benki
zimekosa fedha za kujiendesha, Mafuru alisema taarifa walizozipata ni kwamba
Septemba mwaka huu, benki hizo zaidi ya 50 nchini zimekopesha zaidi ya Sh
trilioni 16.3 kwa watu mbalimbali.
Hata hivyo, alisema kati ya fedha hizo, Sh trilioni
1.43 zimekopeshwa bila ya kurudishwa katika benki husika na kwamba benki hizo
zinashindwa kueleza ukweli uliopo badala yake wanalalamika kwamba hatua ya
serikali kuamua fedha zake zitunzwe BoT badala ya katika benki za kibiashara,
ndio sababu ya hali yao (benki) mbaya.
Kwa mujibu wa Mafuru, serikali imeamua kuchukua
uamuzi huo wa kuzitoa fedha zake kutoka katika benki mbalimbali za kibiashara
nchini kwa ajili ya kuwezesha serikali kujua mapato wanayopata kutoka katika
taasisi zake.
Msajili wa Hazina amesema zaidi ya Sh bilioni 515
zimeingizwa BoT baada ya uamuzi huo wa Serikali ya Awamu ya Tano ambao
ulitangazwa na Rais John Magufuli baada ya kushika madaraka mwaka mmoja
sasa.
Mafuru alikiri kuwa ni kweli kwamba mzunguko wa
fedha umekuwa mdogo na kueleza kuwa chanzo chake si kwamba benki zimekosa fedha
kwa ajili ya kujiendesha.
Alifafanua kuwa awali watu wengi walitegemea safari
na posho ambazo baada ya chenji kubaki, walikuwa wakitumia bila ya malengo,
lakini sio kwamba mzunguko huo wa fedha unawaathiri watu wote.
“Tumeona tusitegemee wahisani badala
yake tujiwekeze katika miradi mikubwa ya maendeleo ambayo kwa sasa
haitaonekana, lakini baadaye itasaidia kuondoa nafasi iliyopo sasa,’’
alisema Mafuru.
“Tayari shilingi bilioni 515 zimeingizwa
BoT na mpaka Septemba mwaka huu fedha hizo zilikuwa kwenye akaunti hiyo. BoT ni
sehemu ya mfumo wa benki, kwani itakuwa inafanya kazi ya kukopesha kama zilivyo
benki nyingine,” alifafanua Mafuru ambaye ofisi yake
inasimamia mashirika na taasisi za umma.
Alifafanua kuwa ofisi yake ambayo ina jukumu la
kusimamia mapato na matumizi, awali walikuwa wanapata shida kupata taarifa za
mapato na matumizi katika benki hizo zilizopo kila kona nchini na kwamba baada
ya BoT kuchukua dhamana hiyo, imewasaidia, kwani wanaandika barua na kupatiwa
taarifa hizo kwa muda mfupi.
Alisema serikali inategemea mapato yake kutoka
katika makundi matatu ambayo ni Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na kupitia
mashirika na taasisi mbalimbali.
Alisisitiza kuwa itasaidia kujua mashirika hayo
zaidi ya 260 namna wanavyotumia fedha zake katika miradi mbalimbali na kwamba
suala la kuchukua fedha bila ya kuzitumia lisiwepo.