Ngariba wa Wakurya Dar Aibuka, Awatahiri Watoto Saa 9 Usiku!
Na Gabriel Ng’osha
TOHARA ni jambo la muhimu na la lazima miongoni mwa vijana wa Kabila la Wakurya, linalopatikana Mkoa wa Mara.
Jambo hili la kimila, kwa kawaida hufanyika Desemba ya kila mwaka,
ambapo vijana wa kike na kiume hufanyiwa tendo hilo linalotafsiriwa kama
kukua kwao.
Kwa
kawaida tohara hufanywa na watu maalum, waitwao mangariba, ambao wazazi
hulazimika kuwapeleka watoto wao kwa wataalam hao ambao hutumia vifaa
vya kijadi huku zoezi lenyewe, likifanyika usiku.
Kutokana
na kusambaa kwa watu wa kabila hilo katika mikoa mbalimbali na ugumu wa
maisha pamoja na umbali uliopo, baadhi wameshindwa kurejea nyumbani
kufanya zoezi hilo, badala yake wameamua kufanyia huko wanakoishi.
Jijini
Dar es Salaam, ambako jamii kubwa ya kabila hilo wanaishi maeneo ya
Kivule na Kitunda, nao wameamua kufanyia tohara huko wanakoishi, lakini
wakienda sawa na wenzao waliopo nyumbani mkoani Mara.
Baada
ya zoezi hilo kufanyika usiku wa manane, mapema asubuhi hufuatiwa na
sherehe kubwa ya kushangiliwa kwa kufanikishwa kwa zoezi hilo,
linaloenda sambamba na washangiliaji kubeba silaha za jadi kama mapanga,
visu, sime na mikuki.
Leo,
mwandishi wetu anakutana na Ngariba, mzee Mwita Matiku ‘Mwita Dokta’
(52), ambaye anafunguka kuhusu suala zima la tohara kwa jamii yake.
“Suala
la kutahiriwa kwa vijana kuanzia miaka 14 na kuendelea kwa jamii ya
Wakurya ni la kawaida sana na hata utaratibu wa kushangilia baada ya
kuwatahiri watoto wetu umekuwepo kwa miaka mingi sana.
“Kwa sisi ambao tuko Dar es Salaam, hatuwezi kufunga safari ya kwenda Mkoa wa Mara kila
mwaka kwa ajili ya kwenda kuwatahiri watoto wetu, hivyo tumekuwa
tukisubiri wazee wa kimila kule Mara wakianza zoezi hilo basi na sisi
tulioko Dar tunaanza.
“Ni
kama sherehe ya kimila ndiyo maana wakimaliza kutahiriwa, wazazi wa
wahusika huamua kufanya sherehe kwa kuchinja mbuzi au ng’ombe kisha
kuwaalika jamaa zao.
“Mara nyingi hutahiriwa majira ya kuanzia saa 9 hadi 11 alfajiri kwa sababu damu inakuwa baridi hivyo haiwezi kuvuja nyingi.
“Nimekuwa
nikiwatahiri vijana wengi sana kwa miaka sita sasa na mwaka jana
nilitahiri vijana zaidi ya 200 ila mwaka huu nimewahudumia vijana 50 kwa
sababu kuna ngariba mwingine ameibuka maeneo haya.
“Wanapotoka
kutahiriwa majira ya alfajiri ndipo hupokelewa na ndugu zao kishujaa
wakiwa na mapanga, mishale, mikuki, fimbo huku wengine wakiwa wamejipaka
damu, wamevaa majani na kadhalika. Hupita mitaani huku wakishangilia
kama alama ya watoto wao kukua na kuitwa wanaume kamili.
“Tohara
yangu mimi ni ya kitaalamu na nina taaluma ya uuguzi, kwani ninafanya
vitu vyote ambavyo hufanywa hospitalini ikiwemo kusafisha vifaa vya
kukatia, kufunga kidonda, kushona, kusafisha kwa kuchemsha vifaa pamoja
na kutumia kifaa kipya kwa kila mtahiriwa.
“Mara
nyingi gharama ya kutahiriwa huwa ni maelewano lakini huanzia shilingi
30,000 kwa kijana mmoja. Mwaka huu kwangu itakuwa ni wa mwisho, inabidi
niwapishe na vijana wafanye kazi hiyo.
“Kwangu
mimi sijawahi kufanya tohara kwa watoto wa kike, kwanza siruhusiwi
kutokana na jinsia yangu na kama wanafanya basi itakuwa ni usiku na kwa
kificho sana maana serikali imepiga marufuku kitu hicho hata jamii yetu
nayo inazidi kuelimika juu ya madhara ya tohara kwa wanawake,” anasema
mzee Mwita.