WAZIRI MPINA: “WAMILIKI WA VIWANDA WALIOJENGA JUU YA MITARO KUSHUGHULIKIWA”
Akiwa katika siku nyingine ya ukaguzi wa
mazingira jijini Dar es salaam, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais
Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Mpina, leo ametembelea katika Maeneo
ya keko Magurumbasi na kujionea namna ambavyo wamiliki wa viwanda
wanavyotiririsha maji katika mfereji maarufu kwa jina la mseleleko.
Baada ya ukaguzi wa mazingira katika
maeneo hayo, Naibu Waziri Mpina amewaasa wawekezaji wenye viwanda nchini
waliojenga juu ya miundombinu ya majitaka kutafuta njia nyingine ya
ujenzi sahihi ya miundombinu ya majitaka kutoka viwandani mwao kwenda
kwenye mfumo wa mamlaka za maji na kuelekeza kuwa iwapo wataonekana
kuziba kwa ujenzi wa majengo yao mitaro mikubwa ya miundombinu ya maji,
sheria itachukua mkondo wake ikiwa ni pamoja na kubomoa majengo yao.
Akijibu swali la mwandishi wa habari wa
kituo kimoja cha television hapa nchini, lilihoji kuusika kwa watumishi
wa umma kwa namana moja au nyigine kiujanja ujanja katika kuruhusu
vibali vya ujenzi na kupelekea uharibifu wa miundombinu ya majitaka na
mazingira kwa ujumla, Mpina alisema kuwa endapo kutagundulika kuwa na
ushiriki wowote wa watumishi wa umma katika suala hilo sheria pia
itachukua mkono wake.
Pamoja na hilo Naibu Waziri Mpina
amewaeleza wenye viwanda wanaoendelea kuchafua mazingira kuwa kutakuwa
na oparesheni kubwa nchini ya ukaguzi wa mazingira itakayohusisha
halmashauri za miji, mamlaka za maji, wamiliki wa mabomba ya maji taka
na wananchi ili kuwajibika kwa pamoja katika kunusuru uharibifu wa
mazingira.
Aidha Ameliagiza Baraza la Taifa la
Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC kuiandikia hati ya zuwio TANROADS
ya mwezi mmoja itayowataka wafumue karavati lao linalopita chini ya
barabara katika eneo la kurasini BP darajani na kuliongeza ukubwa ili
majitaka yaweze kupita kwa nafasi.
Naibu waziri Mpina Pia amewataka
Viongozi wa Manispaa ya Ilala kusimamia kikamilifu usafi wa Mazingira na
kuwataka wananchi wa eneo la keko magurumbasi wanaokaa karibu na
mfereji wa mseleleko kufanya usafi katika mfereji huo na kutooutumia
kama DAMPO.
Kwa upande wake mratibu wa Mazingirawa
kanda ya mashariki kutoka NEMC Bw. Jaffari Chimgege amesema wao kama
Baraza watakaa kwa Pamoja na wawekezaji, wenye makaravati madogo
yanazoshindwa kupitisha majitaka vizuri jijini DSM na kutafuta suluhisho
la kudumu kwani hali hiyo ni hatari hasa katika kipindi cha mvua,
inaweza kusababisha magojwa ya milipuko kama vile kipindupindu.
Naibu
Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina,
akiwa ameongozana na wananchi wanaoishi maeneo ya Keko Magulumbasi
katika ziara ya ukaguzi wa Mazingira.
Naibu
Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina
akimsikiliza Mtaalamu wa Mazingira kutoka NEMC, Jaffar Chimgege katika
ziara hiyo ya ukaguzi wa mazingira jijini Dar es salaam.