Hatari Sana! Vitovu vya Vichanga, Maji ya Maiti Vyauzwa kwa Siri Kubwa, Dar
Na Mwandishi wetu | Gazeti la Uwazi Toleo la Desemba 20, 2016
DAR
ES SALAAM: Hatari! Kuna msemo kwamba, kila mtu anakula anapofanyia
kazi, lakini ulaji mwingine ni wa hatari sana! Mfano huu wa madai
kwamba, baadhi (msisitizo baadhi) ya watumishi kwenye baadhi ya
hospitali na vyumba vya kuhifadhia maiti (mochwari) jijini hapa wamekuwa
wakiuza vitovu vya watoto wachanga na maji yaliyooshea maiti, Uwazi limechimba.
Kwa mujibu wa chanzo, biashara hiyo hufanyika kwa siri kubwa kwani ni kinyume na utaratibu wa utendaji kazi wa hospitali husika.
TWENDE NA CHANZO
Kwa
maelezo zaidi, chanzo kilisema: “Hii biashara jamani imeshamiri sana.
Ila sasa kuizima itakuwa ngumu kwa sababu moja kuu, ni siri sana.
Mnunuaji na muuzaji wanajuana.”
Maji ya maiti yakiuzwa.
BEI YAKE
“Kuhusu
bei ni kama makubaliano. Lakini iko hivi, maji yaliyooshea maiti
ukiyataka kwenye chupa ya lita moja na nusu ni shilingi laki moja
(100,000), ila kama utalia sana, wanashusha hadi shilingi elfu tisini
(90,000).
“Kitovu kimoja cha kichanga ni shilingi elfu themanini (80,000), kama utalia sana mwisho ni elfu sabini (70,000).”
WATEJA WAKUBWA
“Katika
kufuatilia, imegundulika kuwa, wateja wakubwa sana ni waganga wa
kienyeji. Hapa naomba nieleweke. Namaanisha waganga wa kienyeji na si
waganga wa tiba asilia au wa mitishamba. Yaani wale wanaotibu zaidi kwa
kutumia tunguli huku wakiwa wamevaa shanga na mikia ya wanyama.
“Lakini
mbali na wateja wakubwa kuwa waganga, pia wapo watu ambao si waganga
bali wamepewa masharti na waganga. Kuna watu wakienda kwa waganga
kuaguliwa, wanaambiwa ili tatizo liishe, lazima apate maji ya maiti au
kitovu cha mtoto mchanga.
KAZI YAKE KUBWA
“Kazi
kubwa ya hivi vitu ni tiba, kuna waganga wanatumia maji ya maiti
kuagulia watu. Mfano wale wenye kesi kubwa, magonjwa sugu, kuwazindua
watu wanaoonekana kama mazezeta na pia hutumia kukinga mashamba au
biashara isikutwe na mikono ya wabaya.
“Lakini
vitovu vya watoto pia vinatumika kuzindikia nyumba, kuagulia utasa wa
wanawake wanaosumbuka na kuzaa na kuzuia wachawi kuingia ndani ya
biashara au nyumba zile za kifahari.
“Pia vitovu hutumiwa na waganga katika kuwaumiza wanaume wanaotembea na wake za watu. Nasikia kuna dawa, hasa mkoani Tanga,
maeneo ya Handeni inajulikana kama usinga, mwanaume akitembea na mke wa
mtu anakufa mara moja. Sasa nasikia katika dawa hiyo, kitovu cha mtoto
kipo.”
SEHEMU HUSIKA
“Kama
utataka maji yaliyooshea maiti utauziwa na watu wanaofanya kazi
mochwari, ingawa si kila mfanyakazi wa mochwari anajihusisha na biashara
hiyo. Ila wapo. Na kama utataka kitovu cha mtoto, wauzaji wakuu ni
baadhi ya wauguzi wasio waaminifu, ingawa pia si wote,” kilisema chanzo.
MADAI YAFANYIWA KAZI
Ili kupata ukweli au uongo wa madai hayo, Uwazi kwa
kutumia waandishi wake wa kikosi cha Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ wiki
iliyopita lilifanya kazi ya kuzunguka kwenye hospitali ndogo na kubwa
za jijini Dar.
Baadhi
ya hospitali (majina tunayo), wauguzi wake walikuwa tayari kufanya
biashara hiyo licha ya kwamba, walionesha tahadhari kubwa wakati wa
‘kubageini’ bei.
OFM haikufikia hatua ya kununua kwa kuwaambia wahusika itarudi tena, lakini ukweli ukawa umejulikana kwamba, biashara hiyo ipo.
Katika
hospitali moja, OFM ilikwenda mpaka mochwari na kuzungumza kwa siri na
mfanyakazi mmoja wa chumba hicho ambaye alikubali kuuza maji yaliyooshea
maiti kwa gharama ya shilingi 90,000 baada ya kupunguza bei.
Mtu
wa mochwari: “Sikia kijana. Bei ya mwisho kabisa ambayo siwezi
kupunguza zaidi ya hapo kwa maji ya maiti ni shilingi elfu tisini. Kwa
hiyo kama unayo lete pesa nikupe mzigo.”
OFM:
“Sawa, lakini anayehitaji ni kaka yangu, yeye ana kesi, mganga
kamwambia ampelekee maji ya maiti. Ngoja nimpigie ili ikibidi anitumie
pesa kwa mtandao wa simu.”
OFM
alikwenda kusimama pembeni na kuwasiliana na makao makuu ya kitengo
hicho na kupewa maagizo kwamba, aongee na mtu huyo kuwa biashara
ifanyike nje ya mochwari ili OFM iweze kupiga picha za kificho (kama
machale yalimcheza), mhudumu huyo hakuwa tayari.
OFM LASAKA MITAZAMO
Ili
kupata mawazo mbalimbali na angalizo pia, OFM iliwapigia simu baadhi ya
watoa huduma ya utabibu jijini Dar es Salaam, lakini aliyeweza
kupatikana mara moja ni tabibu Maneno Tamba ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Chama cha Waganga wa Tiba Asili Tanzania.
Yeye alianza kwa kuambiwa kuhusu kuwepo kwa biashara hiyo ambapo alionesha kushtuka sana na kusema:
“Kwanza
sijui kama kiungo cha binadamu kinaweza kutumika kutibu. Lakini ni
hatari sana. Mimi kwa upande wangu kwanza sitibu kwa kutumia viungo vya
binadamu wala kitu chochote kinachotokana na mwili wa binadamu.
“Ila
wateja wa hivyo vitu sijui watakuwa akina nani? Maana bwana kuna
waganga, kuna wanga, kuna wachawi na kuna wajanja. Sasa sijui katika
makundi hayo, kundi gani linaweza kununua vitu hivyo lakini huenda
lipo.”
OFM NA WAGANGA WAKUU WA MANISPAA
Pia,
OFM liliwatafuta waganga wa hospitali mbalimbali za jijini Dar. Awali,
lilimtafuta Mganga Mkuu wa Jiji, Judith Kahama lakini simu yake iliita
bila kupokelewa. Na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu ya mkononi
(SMS) na kuambiwa kuhusu madai hayo, hakujibu.
OFM
lilifanikiwa kumpata Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Dk. Victorina
Ludovick ambapo katika mazungumzo yake ana kwa ana na OFM kuhusu kuwepo
kwa madai hayo, alisema:
“Hilo
suala sijawahi kulisikia. Ila kama nyie mnaweza kufanya uchunguzi,
andikeni barua kwa Afisa Habari wa Jiji iende kwa Mkurugenzi wa
Manispaa, akitoa ruhusa mfanye mnaweza kutusaidia pia sisi.”
ANGALIZO
Muuguzi mmoja kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),
alisema kuwa ni vizuri wanawake wanapokwenda kujifungua kuhakikisha
hakuna ujanjaujanja juu ya uhifadhi wa vitovu vya watoto wao.
“Ni
kawaida kwa mzazi kupewa kitovu cha kichanga chake kabla hajatoka
hospitali ili akakifukie mwenyewe anakotaka. Unajua mambo ya kitovu yana
mila na desturi, nasi tunaheshimu hilo. Sasa hao wenzetu wanaouza
vitovu wanavipata wapi? Ina maana huwa hawawapi wenyewe? Mimi nawaomba
akina mama wawe makini,” alisema muuguzi huyo.
OFM, juzi ilimpigia simu Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla ili
kusikia kutoka kwake, lakini simu yake haikuwa hewani. Hata alipopigiwa
waziri mwenye dhamana, Ummy Mwalimu, naye simu yake haikuwa hewani.
Chanzo:GPL