Zinazobamba

Meya wa jiji abaini madudu yanayofanyika na viongozi soko la Kariakoo


 
Meya wa Jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita akisikiliza taarifa inayosomwa na Ofisa biashara soko la Kariakoo wakati wakiwa na wajumbe wa halmashauri ya jiji na menejiment ya soko   baada ya kufanya ziara yake Jana.
 Meya wa Jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita akisisitiza jambo kwa wajumbe wa halmashauri ya jiji  baada ya kupokea taarifa ya  soko iliyokuwa ikisomwa Mbele ya wajumbe wa halmashauri hiyo.




Na Christina Mwagala,Dar es Salaam

ZIARA ya Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita, imebaini kuwepo kwa wizi katika vizimba vya soko la kariakoo jambo ambalo limeonyesha kulinyima jiji mapato kwa kipindi kirefu.
Wizi huo umebainika jana baada ya wajumbe wa kamati ya Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam kufanya ziara ya kukagua mali za jiji ikiwa ni mwendelezo wa ziara zilizowahi kufanyika hapo awali.

Katika kikao hicho ambacho kilifanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Soko la kariakoo, Meneja Mkuu wa Shirika la Soko la Kariakoo  Hetson Kips alisema kwamba shirika hilo linakabaliwa na tatizo la uwezo mdogo wa fedha jambo linafanya kushindwa kumudu kuendeshwa kwa shirika hilo.

Akizungumza katika kikao hicho, Meya wa Jiji Isaya Mwita pamoja na mambo mengine alionyesha kukerwa na hali aliyoiona katika soko hilo na hivyo kumueleza  mejena huyo kwamba asifanye mchezo na ujio huo kwani atafanya kwa vitendo nasio kupita tu.

Isaya alisema anachotaka kukiona ni kwamba wafanye kila njia iya  kuhakikisha kwamba jiji linapata fedha badala ya mchezo mfu wa wizi ambao wanaufanya.
 Alimueleza kwamba, kabla ya kuanza kufanya ziara hiyo anatambua kila kitu ambacho kinafanyika kwenye soko hilo hivyo kupita kwake ni kutaka kutoa ujumbe kwamba yupo na anatambua kinachoedelea.

“ Leo tunaongea kirafiki,  sitaki kuongea sana, sitawawajibisha hata mmoja, ila kunasiku mtajikuta hampo hapa , narudia tena tukienda mbali zaidi kwa wizi huu ambao mnaufanya hali itakuwa mbaya” alisema Meya Isaya.

Alifafanua kwamba, hili jambo halijaisha, siku ambayo nitapita tena halafu nikakuta jiji pesa hazija ingia ,hali itakuwa mbaya, fanyeni jitihada za kuliwezesha jiji lipate pesa, msiseme kwamba hakuna pesa mnaendesha soko kwa hasara wakati ninajua pesa zipo ila mnaliibia jiji.

Awali akisoma taarifa ya soko hilo, Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko Kariakoo, Hetson Kips alisema kwamba wanakabiliwa na tatizo la uwezo mdogo wa kifedha jambo linalofanya kushindwa kumudu shuguli za uendeshaji.

Alisema hali hiyo ndio imefanya  shirika hilo kushindwa kulipa madeni yake kwa wakati na kwamba kwa sasa shirika linakabiliwa na madeni yaliyotokana na huduma mbalimbali zilizofanywa na wakandarasi wa vipindi vilivyopita.

Alisema sheria ya shirika hilo ambayo imeshapitwa na wakati imesababisha baadhi ya wafanyabiashara kukataa kuingia mikataba mipya na hivyo kuwa wagumu kulipa viwango vya vipya vya kodi stahiki vitakavyoendana na wakati sambamba na kukidhi gharama za sasa za kiuendeshaji.

“ Gharama ya viwango vidogo vya kodi ya pango na ada ya soko vimekuwa haviendani na hali halisi ya soko kibiashara , pamoja na jitihada za shirika hili kupandisha viwango kutoka shilingi 8,000 hadi 10,550 ofisi za maduka mwaka 2016 hadi 2017 kwa mita za mraba hadi shilingi 12,500, 14,750 kwa mita mraba kwa imekuwa ni changamoto” alisema Meneja.

Katika taarifa hiyo ilieleza kwamba shirika hilo linamilikiwa na wanahisa wawili ambao ni Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam ambayo inamiliki hisa asilimia 51 ambazo pia hadi sasa hazijalipwa na hazina inayomiliki asilimia 49 na kwamba shirika halipati ruzuku serikalini.

Taarifa hiyo ilionyesha kuwakera wajumbe wa kikao hicho na kumtaka Meneja aache kuwadanganya kwa kuwa ukweli halisi wa jambo hilo wanaujua.

Diwani wa Kata ya Mbezi Hamfrey Sambo alihoji kwamba “ awali mliwahi kusema kwamba jiji halina hisa na leo hii mnasema kwamba jiji linahisa, uhalali huo mmeutoa wapi” alihoji Sambo.

Mbali na hivyo, Sambo pia alisema anatambua kwamba vizimba vya kariakoo havipangishwi kwa bei ambayo wanaizungumza mbele ya wajumbe wa kikao na kwamba kuna mapato makubwa ambayo yanapatikana ila kutokana na ujanja ujanja uliopo ndio umefikia hatua hiyo ya jiji kukosa mapato.

“ Natambua kabisa kwamba hapa mnatupiga pesa nyingi, kuna ujanja ujanja ambao unafanyika , na humu tunajua wapo wakubwa ambao wanavizimba vyao humu, lakini sasa unaposema kwamba kuna hasara ambayo inapatikana hatukuelewi, tunaomba utuambie ukweli” alisisitiza Sambo.

Mejena Hetson alisema kwamba tangu afike hapo anamiezi miwili, na kwamba tayari ameanza kufanya mazungumzo na menejimenti ya soko hilo na kwamba kikao kitakachofanyika kesho kitakuja na majibu ya mkanganyiko huo.

Alisema si jambo hilo tu, lakini pia wapo wafanyabiashara wengine ambao mikataba yao imekwisha lakini wanaendelea kufanyabiashara na mbaya zaidi mikataba hiyo inaonekana kusainiwa mara mbili, jambo ambalo alisema ni changamoto kwao.
Alisema kuwepo kwa hali hiyo kunamfanya kushindwa kuchukua maamuzi, huku wakati mwigine akifikiri kuvunja kwa mikata ya wafabiashara hao  ili apangishe wengine.

Kwa upande wake Diwani wa kata  ya Tandika  Mariam Mtemvu alishauri kwamba ili kuepukana na hali hiyo, ni vema uongozi huo ukafanya kazi ya kutembelea wafanyabiashara waliopo kwenye vizimba hivyo na kuingia nao mkataba badala yawale ambao wanakuja kufanya mazungumzo nao kwani kufanya hivyo kutapunguza hali ya wizi wa mapato.

“ Mfanye jambo watu ambao wanakuja kuomba vizimba tunafahamu kwamba nawao wanapangisha watu, sasa ili kuondoa hili na jiji likapata mapato, wazungukieni wote ambao wanafanya biashara hapa, muongee nao ndio hao muwape mikataba.
Nao watakubali kodi kuongezeka, hawa ambao wanakataa tayari walishawapandishia wenzao kodi tofauti na ile ambayo mliwaelekeza, sasa hawawezi kurudi kuwaambia kwamba kodi imepanda.