SERIKALI YAWANYIMA RASMI MIKOPO WANAFUNZI WANAOSOMA NCHINI CHINA,SOMA HAPO KUJUA
Watanzania waliopata ufadhili wa kusoma nchini
China, hawatapata mikopo baada ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HESLB) kuwaondoa kwenye orodha ya wanufaika.
Taarifa iliyotolewa na HESLB, ikijibu Ubalozi wa
Tanzania nchini China, kuhusu madai ya kuchelewa kwa fedha za mikopo kwa
wanafunzi wanaosoma nchini humo imeeleza kuwa hatua hiyo inatokana na maelekezo
ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwamba wanafunzi wote wanaopata
ufadhili kutoka nchi rafiki watajitegemea ikiwamo gharama za tiketi za ndege.
Barua hiyo ya Desemba 20, 2016 iliyomnukuu
Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul Razaq Badru inaeleza kuwa mwaka huu
wanafunzi hao hawatanufaika na mikopo kama ilivyokuwa ikitolewa miaka ya nyuma.
Jana, akizungumza na waandishi wa habari, Badru
aliitambua barua hiyo huku akisita kutolea ufafanuzi wake kwa madai ilikuwa ni
majibu kwa wanafunzi hao wa China.
Hata hivyo, alisema endapo kutakuwa na madai kutoka
kwa wanafunzi hao watalazimika kutolea ufafanuzi.
Akizungumzia suala hilo Naibu Waziri Elimu, Stella
Manyanya alisema ni hekima zaidi kuangalia au kusaidia wanafunzi wa ndani
wasiokuwa nacho kuliko wanaopata ufadhili wa nje ya nchi.