MAAMBUKIZO MAPYAA YA VVU NA UKIMWI YASHUKA,BOSI WA TACAIDS ATAJA SABABU YAKE,SOMA HAPO KUJUA
Mkurugenzi
Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) Dk.Leonard Maboko
(katikati), akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es
Salaam leo, wakati akitoa taarifa kuhusu mapambano dhidi ya ugonjwa wa
ukimwi katika mkutano wa kujitambulisha kwao tangu ateuliwe na Rais
Dk.John Magufuli kushika nafasi hiyo Julai 7 mwaka huu. Kutoka kushoto ni
Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Muitikio ya Kitaifa, Dk.Hafidhi
Amri, Mkuu wa Kitengo cha Sheria Tacaids, Elizabeth Kaganda na Mkurugenzi wa
Habari na Ulaghibishi, Jumanne Issango
|
MAAMBUKIZO Mapya ya VVU na Ukimwi yameshuka nchini
kwa zaidi ya asilimia 20 kati ya mwaka 2010 na 2015 imefahamika.
Hayo yalielezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya
Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) Dk.Leonard Maboko wakati akitoa
taarifa kwa waandishi wa habari katika mkutano wa kujitambulisha kwao
tangu ateuliwe na Rais Dk.John Magufuli kushika nafasi hiyo Julai 7 mwaka
huu.
Amesema maambukizo mapya ya VVU yaliyokadiriwa kuwa
watu milioni 2.1 kwa mwaka 2015 Duniani kote wakati maambukizo mapya yameshuka
kwa asilimia 50 miongoni mwa watoto duniani.
Alisema watoto 290,000 wapya waliambukizwa mwaka
2010 na watoto 150,000 waliambukizwa mwaka 2015 ambapo maambukizo mapya
kwa watu wazima hayajashuka tangu 2010 duniani.
Katika hatua nyingine Dk. Maboko alisema Tafiti
zimeonesha kuwa wanawake ndio waathirika wakubwa wa maambukizo ya
VVU kwa upande wa Tanzania Bara ukilinganisha na wanaume.
Alisema maambukizo VVU kwa upande wa Tanzania Bara
ni asilimia 5.3 wanawake wakionesha kuathirika zaidi kwa asilimia 6.2
ukilinganisha na wanaume ambao ni asilimia 3.8.
"Katika utafiti huo wa mwaka 2011 na 2012
ulionyesha kuwa Mkoa wa Njombe ulikuwa na kiwango kikubwa cha maambukizo
ukiwa na asilimia 14.8 ukifuatiwa na Iringa kwa asilimia 9.1 na Mbeya kwa
asilimia 9" amesema Dk.Maboko.
Dk.Maboko amesema Mkoa wa Manyara ulikuwa na kiwango
kidogo cha maambukizo ya asilimia 1.5 lakini takwimu za ndani ya mkoa huo eneo
la Mirelani kwenye mgodi wa Tanzanite maambukizo ya VVU yalikuwa ni
asilimia 16 kiwango ambacho ni cha juu ya Mkoa wa Njombe.
Dk. Maboko amewaomba wananchi kote walipo
kutobweteka kwa mafanikio yaliyo ya mapambano dhidhi ya VVU na ukimwi na kuwa
yawe endelevu hata katika maeneo au mikoa ambako kuna maambukizo kidogo ya VVU.
Amesema kama nchi tunatakiwa kuweka nguvu nyingi
kifedha na kimkakati katika maeneo na makundi yenye kiwango kikubwa cha
maambukizo ya VVU ikiwa ni pamoja na kuimarisha utafiti na ukusanyaji wa
takwimu za VVU na Ukimwi ili tuendelee kubaini na kupanga mipango dhidi
ya ugonjwa huo inayoongozwa na takwimu.
Ameongeza kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloratibu mapambano dhidi ya Ukimwi (UNAIDS) limeweka malengo ya muda wa
kati ya tisini tatu (90-90-90). 90 ya kwanza ikimaanisha asilimia tisini ya
watu wote wanaokisiwa kuwa na VVU kujua hali zao na 90 ya pili ikimaanisha
kuwa asilimia tisini ya waliobainika kuwa na VVU kuanza kutumia dawa za
kupunguza makali
ya VVU (ARV) mara moja na 90 ya tatu ya walioanza
dawa waweze kuwa na ufubazo endelevu wa virusi vya ukimwi mwilini mwao.
Dk. Maboko alitoa mwito kwa wananchi, Taasisi za
kijamii, Serikali, watu binafsi na makampuni ya kibiashara kuchangia mfuko wa
udhamini wa masuala ya ukimwi (AIDS TRUST FUND-ATF) ulioanzishwa na serikali
ili kuondokana na utegemezi kwa wafadhili.