CUF YAIACHIA CHADEMA KATA ZOTE ZA UDIWANI KWENYE UCHAGUZI MDOGO,SOMA HAPO KUJUA
Shaweji Mketo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF
(kushoto)
|
CHAMA cha Wananchi CUF kimesema hakijasimamisha
mgombea yoyote katika chaguzi za marudio zinazotarajiwa kufanyika Januari 22
mwakani katika kata 20, ananadika Pendo Omary.
Akizungumza
na MwanaHALISI Online leo jioni Shaweji Mketo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF
amesema hatua hiyo inatokana na mgogoro unaondelea ndani ya chama hicho.
Mgogoro unaoendelea ndani ya CUF ni juu ya Prof.
Lipumba aliyejiuzulu uenyekiti wa chama hicho Agosti 2015 lakini Juni 2016
akatangaza kutengua uamuzi wake na kuirejea nafasi hiyo huku uongozi wa CUF
chini ya Maalim Seif ukipinga na hatimaye kumvua uanachama lakini ameendelea
kutambulika na Msajili wa Vyama vya Siasa.
Mketo amesema hapo awali CUF ilikutana na vyama
washirika katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) – Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), NCCR – Mageuzi na National League For Democracy (NLD) ili
kujadili namna vyama hivyo vitavyoshiriki katika uchaguzi ikiwemo kuachina
kata.
“Sisi CUF tulikutana na vyama washirika wa ukawa
katika kamati ndogo ya ufundi ya Ukawa ambapo tulikubaliana mambo kadhaa kuhusu
kuachiana kata.
Wakati tukijiandaa kuzungumza na waandishi wa habari
kuhusu ushiriki wa Ukawa katika uchaguzi wa marudio, ghafla akajitokeza Magdalena
Sakaya (Mbunge wa Kaliua – CUF ambaye ni mfuasi wa Prof. Lipumba) na kutangaza
kuwa CUF itasimamisha wagombea katika kata zote,” amesema Mketo.
Ameongeza kuwa, “Ieleweke kuwa hatujasimamisha
wagombea sehemu yoyote na Sakaya na wenzake kutangaza kusimamisha wagombea
katika kata zote ni utekelezaji wa kazi zao za kukisaidia Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kupata ushindi.”