WAZIRI MKUU AMLILIA SAMWEL SITTA KITOFAUTI,SOMA HAPO KUJUA
SERIKALI imekiri kwamba pengo la Spika mstaafu,
Samuel Sitta ni kubwa na kamwe halitazibika ndani ya serikali, chama na jamii.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
wakati akitoa salamu za Rais John Magufuli na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan
kwenye maziko ya Spika huyo yaliyofanyika kitongoji cha Mwenge, Urambo mkoani
Tabora jana.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema kama serikali wamepata
pigo kwa kumpoteza mtu muhimu serikalini. Majaliwa alisema, kuondokewa na mzee
Sitta ni pengo kubwa na kamwe halitazibika ndani ya serikali, chama na jamii
kwa ujumla kutokana na mchango wake wakati wa uhai wake.
Pamoja na kutoa pole kwa familia, aliisihi wao
pamoja na wana Urambo kwa ujumla kuupokea msiba huo kwa mikono miwili, licha ya
ukweli kuwa kifo siku zote huwa hakizoeleki.
Akifafanua zaidi jinsi taifa lilivyonufaika Waziri
mkuu huyo alisema, Sitta akiwa mtumishi wa serikali atakumbukwa kwa mazuri yake
kwani alikuwa mtumishi aliyetukuka, mpenda amani, msikivu na aliyependa
kushirikiana na jamii.
Alisema uongozi wake ulikuwa mfano wa kuigwa na
viongozi na jamii kwa ujumla na kwamba kila kazi ambayo alipewa hakusita
kuipokea na wala hakuwahi kuishindwa.
Majaliwa alisema binafsi asiwe mchoyo wa fadhila,
kwani alimfundisha kazi kipindi ambacho yeye alikuwa mkuu wa wilaya ya Urambo
na Sitta akiwa mbunge wa jimbo la Urambo na Spika wa Bunge la Tisa.
“Mara kadhaa alikuwa akikaa nami pale juu ghorofani
nyakati za usiku saa mbili na kunifundisha kazi…..lakini alinionya kuwa
nisipende kujihusisha na migogoro ya watu na alinitaka kupenda kazi kamwe
nisiwe mvivu,” alisema.