Zinazobamba

SAKATA LA ESCROW SASA LAWA PASUA KICHWA,TANESCO YAENDELEA KUNG'ANG'ANIWA,SOMA HAPO KUJUA



Benki ya Standard Chartered Limited ya Hong Kong (SCB-HK) imefungua maombi Mahakama Kuu ikitaka, pamoja na mambo mengine, Shirika la Umeme (Tanesco) lizuiwe kuilipa kampuni ya uzalishaji nishati hiyo ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Badala yake, SCB-HK inaomba malipo hayo yahifadhiwe mahakamani hapo hadi Tanesco itakapolipa dola 148 milioni za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh320 bilioni) kwa benki hiyo kama Mahakama ya Kimataifa ya Utatuzi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) ilivyoagiza mwezi Septemba, tofauti na ilivyokuwa wakati wa mgogoro wa Tanesco na IPTL wakati fedha zilipowekwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).


Uamuzi wa ICISD ulikuja takriban miaka mitatu baada ya Serikali kuidhinisha malipo ya takriban Sh306 bilioni kutoka akaunti ya escrow iliyofunguliwa na Tanesco kwa kushirikiana na IPTL kusubiria uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu mgogoro wa malipo ya tozo ya uwekezaji.
Mwaka 2005 SCB-HK, ilinunua deni ambalo benki ya Danaharta ya Malaysia ilikuwa ikiidai IPTL baada ya kampuni hiyo kukopa dola 101.7 milioni za Kimarekani ili kununua mtambo wa ufuaji umeme wa Tegeta wenye uwezo wa kuzalisha megawati 100. Lakini wakati fedha hizo zilipotolewa, ililipwa kampuni ya Pan African Power Solutions (PAP), jambo lililofanya SCB-HK kufungua kesi hiyo ICSID ikidai ndiyo iliyostahili malipo hayo, kesi ambayo benki hiyo ilishinda.
Umuzi huo wa ICSID umeshakubaliwa na kusajiliwa na Mahakama Kuu Tanzania kupitia maombi namba 687, ya mwaka 2016, yaliyofunguliwa na SCB-HK, na hivyo unatambulika kama uamuzi wa mahakama hiyo.
IPTL inafua umeme ambao unauzwa kwa Tanesco.
Lakini SCB-HK imewasilisha maombi kwa hati ya dharura ikiomba mahakama iizue Tenesco kuendelea kuilipa PAP, ambayo inamiliki IPTL na badala yake pesa hizo ziwe zinahifadhiwa mahakamani hapo hadi deni hilo litakapolipwa lote